Wajawazito Wanging'ombe wadai kukodi wanaume kwenda nao hospitali

Muktasari:

Wajawazito katika Kijiji cha Makoga kilichopo wilayani Wanging'ombe wamedai kuwa wanalazimika kuwakodi wanaume kutoka katika vijiji jirani ili kuwasindikiza kliniki na kuwalipa fedha kutokana na waume zao kukata kwenda nao wakihofia virusi vya Ukimwi.

Njombe. Wajawazito katika Kijiji cha Makoga kilichopo wilayani Wanging'ombe wamedai kuwa wanalazimika kuwakodi wanaume kutoka katika vijiji jirani ili kuwasindikiza kliniki na kuwalipa fedha kutokana na waume zao kukata kwenda nao wakihofia virusi vya Ukimwi.

Kauli hiyo wameitoa leo kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi ambayo kiwilaya yalifanyika katika kijiji hicho.

Wamesema hali hiyo ya hofu ya kupima inatokana na waume zao kuwa na ndoa za wake wengi hivyo kuwajengea hofu ya kupima VVU.

Wamesema ipo haja ya Serikali kuingilia kati suala hilo kwa kuwafungulia mashtaka wanaume wanaowatelekeza wake zao kipindi cha mimba na kwenda kuishi na wanawake wengine kwa kuhofia kupima.

Baadhi ya wanawake hao akiwemo, Visia Chapile amesema huwa wanawakodisha waendesha bodaboda ili aweze kupokelewa na kupatiwa huduma katika kituo cha afya.

"Namchukua bodaboda namlipa hela yake naenda naye kupima kama yule ni mume wangu wakati siyo ili tuweze kupokelewa” amesema.

Naye, Athelimo Mwinuka amebainisha kuwa kuna wanaume wengine wanakubali kwenda na wake zao hospitalini lakini wengi hawakubali.

"Siku za ujauzito ndiyo kuna wanaume wanapima lakini walio wengi huwa wanakimbia" amesema Mwinuka.

Tunapofanikisha watu wengine kupimwa lakini wengine hawapendi kabisa ndio maana inafika mahali wanakimbia”

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Makoga, Dk Peter Tamata wanaume  wengi wa kijiji hicho wamekuwa na mitara jambo ambalo anadhani limekuwa likiwapa hofu kwenda na wake zao kliniki kupima afya kipindi cha ujauzito

“Wanaume wengi wanakimbia pindi wanapo mpa mama ujauzito hii hupelekea akina mama kwenda kuchukua wanaume wengine kusimama badala ya yule mhusika aliyempa mimba” alisema Dk Peter.