Wakamatwa kwa tuhuma za kuwinda twiga

Watuhumiwa wakiwa na nyama ya twiga waliyokamatwa nayo.

Muktasari:

  •  Watuhumiwa hao, wamekamatwa kutokana na operesheni ya kupambana na ujangili katika eneo hilo.

Babati. Kikosi maalum cha kupambana na ujangili katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya wanyamapori ya Burunge wilayani Babati Mkoa Manyara, kimewakamata watu wawili katika Kijiji cha Vilima Vitatu wakituhumiwa kuwinda twiga kinyume cha sheria.

Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) lipo katikati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Manyara na lina eneo kubwa la mapito ya wanyamapori (shoroba) na sasa kuna idadi kubwa ya twiga kutokana na kuimarika kwa uhifadhi.

Kamanda wa Polisi Mkoa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi George Katabazi akizungumza na Mwananchi leo Februari 3, 2023 amesema watuhumiwa hao, wamekamatwa kutokana na operesheni ya kupambana na ujangili katika eneo hilo.

Amewataja waliokamatwa ni Athuman Issa Misanya (23) mkazi wa Mamire na Paul Himid John (23) wilayani Babati mkoa wa Manyara.

"Tunawashirikiana na Jumatatu kama taratibu zikikamilika tutawafikisha mahakamani," amesema.

Kamishna Msaidizi wa mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Peter Mbanjoko akizungumzia tukio hilo, amewaonya wanaojihusisha na ujangili kwani hawapo salama.

"TAWA kwa kushirikiana na polisi na askari wa Burunge WMA Chemchem na TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa), tutaendelea kuimarisha ulinzi katika eneo la Burunge WMA na mengine na hakuna jangili ambaye atasalimika," amesema.

Amesema watuhumiwa hao ambao tayari wamefikishwa polisi Babati mjini jana, wamekamatwa pamoja na vielelezo vya nyama ya twiga ambayo imekutwa katika mifuko, pikipiki moja yenye namba MC361EDY iliyokuwa imebeba nyama hiyo.

"Pia Kuna vitu vingine vingi vya ujangili ambavyo tumewakamata navyo," amesema bila kufafanua.

Naye mwanasheria wa TAWA, Getrude Kariongi amesema katika operesheni hiyo pia, mtu anayetuhumiwa kuwa mnunuzi wa jumla wa nyama ya twiga ambaye ndiye amekuwa akisambaza mitaani, amekamtwa baada ya kutajwa na watuhumiwa waliokutwa na nyama.

Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Babati mkoa Manyara, Emmanuel Laizer ametaka wananchi wa wilaya hiyo kutojihusisha na ujangili kwani ni uhujumu uchumi na lazima watakamatwa.

Uwindaji wa Twiga katika eneo hilo imekithiri kutokana na biashara ya magendo ya nyamapori hata hivyo Taasisi ya Chem chem kwa kushirikiana na TAWA, Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Burunge WMA wamekuwa na operesheni za mara kwa mara kusaka majangili.

Katika operesheni hizo zaidi ya milioni 450 kila mwaka zimekuwa zikitolewa na Taasisi ya Chem chem Association ikiwemo pia kuwezesha mafunzo kwa askari wa wanyamapori eneo la Burunge.