Wakazi Serengeti wamshushia mzigo wa kero Kinana, azijibu

Muktasari:

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM (Bara), Abdulrahman Kinana ameendelea na ziara mkoani Mara ya ujenzi wa chama

Mara. Wananchi wa Wilaya ya Serengeti wamewasilisha kero tano zinazowasumbua ikiwamo kutotekelezwa ujenzi wa Barabara ya Sanzati Nata huku wakikiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) kuweka msukumo wapate suluhu.

Changamoto zingine, mgogoro wa ardhi kati ya wilaya hiyo na Wilaya ya Bunda, mgogoro mipaka baina yao  na hifadhi,kutaifishwa mifugo na vijana wao kukosa ajira katika Hifadhi ya Serengeti.

Kero hizo zinazowasumbua ziliwasilishwa mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana baada ya kutoa fursa ya kuwasikiliza katika mkutano wa ndani uliofanyika Mji wa Mugumu uliopo katika wilaya hiyo.

Kero ya barabara ilianza kuwasilishwa na Mwenyikiti wa CCM, Wilaya ya Serengeti Mnobanda Japani na kusema iwapo itakamilishwa kwa wakati itakuwa njia rahisi kwao kuwashawishi wananchi kuipigia kura katika uchaguzi unaokuja.

"Barabara hii inaanzia Sanzati Nata hadi Arusha inategemewa na wakazi wa Serengeti kwenda hadi Arusha ina kilomita 40 na tuliitumia kuomba kura  kwa wananchi wakati wa uchaguzi uliopita lakini hadi tunakaribia uchaguzi mwingine  ujenzi wake bado unasuasua,tunaomba kiongozi wetu ulibebe jambo hili utusaidie," amesema Japani.

Amesema barabara hiyo ni siasa ya Serengeti na ni changamoto inayolalamikiwa na wananchi wao, hivyo kutokutekelezwa kwake inaweza kuwa kikwazo cha kuwakosesha kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na mkuu.

Amesema kila mwaka barabara hiyo imekuwa ikiwekwa kwenye bajeti lakini ukamilishwaji wake umekuwa ukipigwa danadana nyingi jambo linalowakosesha viongozi walioshika hatamu kuonekana mbele ya wananchi wanaushawishi.

Japani ametaja changamoto nyingine ni mgogoro wa ardhi kati ya wilaya hiyo na Bunda, unaowasumbua kwa zaidi ya miaka 50 waliuwasilisha kwa viongozi lakini wameshindwa kupata suluhu ya kudumu.

"Tunaomba mgogoro umalizike ili watu tuishi vizuri na tuendelee kuheshimiana sote kama jamii moja kwa kuwa watu wameoana kutoka Bunda kuja Serengeti na watu wa Serengeti wameoa Bunda tunaomba utusaidie," amesema Japani.

Changamoto ya mipaka kati ya wananchi iliibuliwa na Diwani wa Machochwe, Joseph Mhegete aliyesema wananchi wake wamekuwa wakikamatwa,kuawa na mifugo yao inataifishwa. 

"Na watu wamekuwa wakipotea mazingira ya kutatanisha na hatujui kwanini tatizo hili linatokea hasa Kwa sisi tunaoishi pembezoni mwa hifadhi hii," amesema.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dk Vicent Mashinji amekiri kuwepo kwa mgogoro hiyo kwa pande zote wananchi na hifadhi.

"Bado tunajitahidi kutoa elimu kwa wananchi kuwataka wasiingie kwenye hifadhi na maofisa hifadhi wanaojichukulia sheria mkononi tumeagiza wachukuliwe hatua za kinidhamu," amesema.

Mkazi wa Molotonga, Rechael Wachota amesema licha ya Hifadhi ya Serengeti  kutangaza nafasi za ajira lakini vijana wanaozunguka eneo hilo hawanufaiki na zimekuwa zikichukulia na watu wengine.

"Sisi wananchi tunashangaa inakuwaje tunazunguka hifadhi hii lakini ajira zikitangazwa zinachuliwa na watu kutoka maeneo mengine wakati sisi tuna vijana wenye sifa," amesema.

Akijibu maswali hayo akianza na mgogoro wa ardhi kati ya Serengeti na Bunda, Kinana amesema atakwenda kuongea na viongozi wa mkoa kupata suluhu huku akiwaomba wazee wa pande zote kukutana kusaidia kutatua.

"Katika hili wazee wakae watushauri na tatizo hili itabidi tutafute namba mzuri ya kutatua kwani njia inayotumika si mzuri maana haiwezekani kwa muda wote huo ishindikane, hivyo wilaya na mkoa wakae waone njia gani wanaweza kutatua," amesema Kinana

Kuhusu mgogoro wa mipaka na hifadhi, Kinana amesema Serikali imeunda kamati ndogo ya kitaifa itakuja kufuatilia mgogoro wa mipaka kati ya wananchi wa wilaya hiyo na hifadhi ya Serengeti.




"Hakuna mtu mwenye haki ya kuondoa haki ya mtu ya kuishi, isipokuwa kama mtu akikamatwa hifadhini anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria," amesema.

Kinana amesema mtu akifanya makosa kuna chombo vya sheria vinavyopaswa kushughulikia na si watu kujichukulia sheria mkononi huku akiwaomba wananchi kuheshimu mipaka.

Kuhusu barabara amesema alishaongea na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa atakuja kuangalia na kuona kumkabidhi mkandarasi mwingine kukamilisha ujenzi wake.

"Tatizo lilipo mkandarasi aliyepewa kazi alikuwa anachelewesha kutokana na kutekelezwa miradi mingi lakini amepunguziwa, hivyo atakuja kuangalia na kuona namba ya kumpata mwingine kujenga," amesema.