Wakazi wa Hai wafurika kumpokea Mbowe
Muktasari:
- Maelfu ya wananchi wa Kilimanjaro na viunga vyake wamejitokeza kwa wingi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) kumpokea mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Hai. Maelfu ya wananchi wa Kilimanjaro na viunga vyake wamejitokeza kwa wingi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) kumpokea mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mbowe kwenda Hai tangu atoke gerezani Machi 4, mwaka huu ambako alikaa kwa miezi minane akikabiliwa na tuhuma za ugaidi na uhujumu uchumi.
Kesi hiyo ya Mbowe na wenzake watatu iliyokuwa ikiendeshwa katika Mahakama ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi ilifutwa baada ya Mandesha Mashtaka Nchini (DPP), kupeleka hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka hayo.
Tangu alipotoka Mbowe, amekuwa akifanya mikutano mbalimbali ikiwemo kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alimuita Ikulu jijini Dar es Salaam na kukubaliana kufanya siasa za kistaarabu na kujenga Taifa
Katika mapokezi ya leo, shughuli mbalimbali zilisimama kwa muda wakati msafara wa Mbowe ukitoka uwanjani KIA kuelekea usawa wa Bomang'ombe ambapo wananchi walisimama kwa wingi.
Mbowe wakati anaondoka uwanja wa ndege msafara wake ulikuwa ukiongozwa na mbwa aliyekuwa ameshikiliwa na kijana mmoja.
Wananchi hao wakiwa na usafiri wa bodaboda, bajaji, magari na wengine wakitembea kwa miguu, walijikusanya katika njiapanda ya Kia Moshi huku Jeshi ka Polisi likiimarisha ulinzi na kuongoza msafara huo.
Alipofika katika Eneo hilo, Freeman Mbowe ambaye alikiwa kwenye gari la wazi akiwapungia wananchi na kuwashukuru kwa kusema "asanteni kunipokea tupo pamoja" kisha msafara kuondoka kuelekea Bomang'ombe zilipo ofisi za Chadema kisha kuelekea Machame ambapo atapokelewa na wazee.
Mapokezi hayo yalisababisha baadhi ya barabara kufungwa kwa muda kutokana na wingi wa watu, magari na pikipiki .