Wakulima malighafi za kutengenezea bia kupigwa jeki

Muktasari:
- Ripoti ya 'Tanzania in Figures 2022' inaonyesha ongezeko la uzalishaji bia nchini kutoka lita milioni 380 mwaka 2021 hadi lita milioni 456 mwaka 2022.
Dar es Salaam. Wakati Ripoti ya 'Tanzania in Figures 2022' inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ikionyesha uzalishaji bia nchini ukiongezeka mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2021, wadau wa sekta hiyo wamekuja na mbinu kuhakikisha bidhaa hiyo ya starehe inazidi kuongezeka.
Takwimu hizo zinaonyesha mwaka 2021 uzalishaji wa bia ulikuwa ni lita milioni 380 kisha kuongezeka hadi kufikia lita milioni 456 mwaka 2022, licha ya kuwapo kwa panda shuka inayodaiwa kuchangiwa na upatikanaji wa malighafi.
Akizungumza katika Maonyesho ya Nane Nane mkoani Dodoma leo Agosti 8, 2024 Ofisa Kilimo wa Kampuni ya uzalishaji bia ya Tanzania Breweries Limited (TBL), Jacob Mwavika amesema ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo wanawawezesha wakulima wa malighafi zinazotengeneza bia ili kuongeza tija.
“Kwa muda mrefu, tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali za kuwasaidia wakulima wadogo hapa nchini ikiwamo kutoa mafunzo ya kitaalamu, vifaa vya kilimo na pembejeo muhimu kwa wakulima.
"Pia, tumefanikiwa kuingia mikataba na wakulima wengi ambao mazao yao yanatumika katika utengenezaji wa bia katika kiwanda chetu ili tuongeze tija na uzalishaji," amesema na kuongeza Mwavika.
Malighafi zinazohusika katika utengenezaji wa bia na vileo vingine ni pamoja na mazao ya: Shayiri, mtama na zabibu.
Katika hatua nyingine, TBL imeandaa mipango ya kuendelea kuwa karibu na kuimarisha uhusiano na wakulima kwa kuongeza ushirikiano katika nyanja za kilimo. Kampuni pia inamikakati kuendeleza miradi ya maendeleo ya kilimo ambayo itaendelea kuboresha hali ya maisha ya wakulima na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.