Wakulima wa tumbaku 870 wapewa motisha mbegu za mahindi

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku nchini, Stan Mnozya (wapili kulia) akimpongeza mkulima Albert Mtunda (wakwanza kulia) baada ya kumkabidhi kilo 10 za mbegu ya mahindi. Picha na Robert Kakwesi.

Muktasari:

Wakulima 870 waliolima tumbaku kwa tija katika Wilaya 29 zinazolima zao hilo nchini wamezawadiwa mbegu za mahindi na Bodi ya Tumbaku (TTB) ili walime kwa ajili ya chakula badala ya kununua kwakutumia mapato ya tumbaku.

Tabora. Wakulima 870 waliolima tumbaku kwa tija katika Wilaya 29 zinazolima zao hilo nchini wamezawadiwa mbegu za mahindi na Bodi ya Tumbaku (TTB) ili walime kwa ajili ya chakula badala ya kununua kwakutumia mapato ya tumbaku.

Wakulima hao waliopata kilo 10 za mbegu ya mahindi kwa kila mmoja mbali na kupata kilo nyingi za tumbaku na kuuza kwa wastani wa Dola kuanzia 2.5 hadi 2.8 sawa na zaidi ya Sh6,000 kwa kila kilo moja, pia walikuwa na mashamba ya miti na mabani ya kutosha.

Akizungumza leo Jumatatu Novemba 20, 2023; Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Stan Mnozya amesema kila wilaya wamepatikana wakulima watatu lengo likiwa ni kuwafanya kuwa na uhakika wa chakula na sio kutegemea  pesa za mauzo ya tumbaku kukinunua badala yake fedha hizo zifanye shughuli zingine za maendeleo.

"Tunataka kuwajengea utaratibu wa kuachana na fedha za mauzo ya tumbaku kununua chakula ili mapato yatokanayo na tumbaku yaendeleze zao hilo na uchumi wa mkulima mwenyewe,”amesema

Mnozya amebainisha kuwa katika utoaji mbegu watahakikisha wanapata wakulima wanaofanya vizuri na kutimiza vigezo vilivyowekwa na bodi ikiwemo upandaji wa miti kwa maana ya kutunza mazingira na kuwa na mabani ya kutosha ya kukaushia tumbaku.

Pamoja na kutoa mbegu za mahindi, Mnozya amesema wamepeleka taarifa kwa wakulima wote wa tumbaku zaidi ya 49,000 nchini kujiandikisha na kutoa mahitaji yao ili wapate mbegu za alizeti bure.

Mnozya amesema bodi hiyo ipo mbioni kuwapanga wakulima kwa makundi ya wakulima wakubwa,  wa kati na wakulima wadogo ambapo vigezo vitakavyowekwa vitajadiliwa mwezi ujao.

Wakiwakilisha wenzao waliopata mbegu hizo, Albert Mtunda mkulima wa Tutuo  Sikonge aliyepata kilo 82,000 ameshukuru utaratibu huo akisema utawafanya wakulima kutowazia kununua mahindi kutokana na fedha za tumbaku.

"Kuna kipindi wakulima walikuwa wanapata shida kwa kutokuwa na chakula huku tumbaku mauzo yake yakichelewa kutolewa," amesema

Juma Ramadhan aliyepata kilo 19,600 naye amepongeza utaratibu huo kuwa utawafanya wakulima wawe na uhakika wa chakula hata kama malipo ya tumbaku yanachelewa.