Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima wadogo Tanzania waomba mikopo kujikita kwenye umeme jua

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiweka nguvu katika kilimo cha umwagiliaji ili kuachana na utegemezi wa msimu wa mvua, baadhi ya wakulima wadogo walio mbali na skimu za umwagiliaji wameomba mikopo ya mifumo ya umeme jua kwa ajili ya kuwezesha umwagiliaji.

Hiyo ni kutokana na kuwa na uwezo wa kupunguza gharama ufanyaji wa kilimo na kuondoa ulazima wa wao kununua mafuta kila siku kuendesha mitambo ikiwemo jenereta kuzalisha umeme.

Haya yanasemwa wakati ambao tafiti iliyofanywa na Taasisi ya African Center for Media Excellence (ACME) imeonyesha kuwapo kwa unafuu wa gharama na ongezeko la faida kwa watu wanaotumia umeme jua kama nishati ya kusukuma maji kwa ajili ya kilimo umwagiliaji badala ya mafuta.

Tafiti hiyo iliyohusisha wakulima 400 kutoka Tanzania na Uganda wanaotumia pampu za kusukuma maji za umeme jua kwa kati ya miezi 4 hadi 5 zinaonyesha kuwa asilimia 91 walishuhudia kupungua kwa gharama katika matumizi huku wakikiri kupata mazao zaidi kutokana na kutotegemea msimu.

Akizungumza na Mwananchi, Denis Mwanja ambaye ni mkulima anayetumia mafuta katika umwagiliaji, amesema umeme jua una gharama nafuuu lakini, ili mtu aweze kuutumia anahitaji kuwa na kiasi kikubwa cha fedha cha kuanzia.

“Ili uwe na nguvu kubwa unahitaji sola panel nyingi zaidi, hii itakufanya uwe na uhakika lakini wengi sisi ni wale wakulima wadogo tusiokuwa na uwezo wa kumudu kuanzia Sh2 milioni kwa wakati mmoja, kama benki zingejikita kukopesha ingetusaidia,” amesema Mwanja.

Amesema licha ya kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa muda mrefu ila matumizi yake ya jenereta yamekuwa yakitegemea siku ambazo ana hela.

“Kama sina hela nitabeba watoto wangu tutamwagilia kwa ndoo hadi tumalize, mikopo ambayo ingetuwezesha kulipa kidogo kidogo kupitia benki ingekuwa nafuu kwa sababu hata hizi kampuni nazo wakati mwingine riba zake ni kubwa,” anasema Mwanja ambaye anakiri kuwa bado hajafikiwa na kampuni za ukopeshaji sola.

Maneno yake yanaungwa mkono na Martha Mzee ambaye ni mkulima wa mbogamboga jijini Dar es Salaam ambaye kiu yake ni kupata mkopo wa pampu isiyotumia umeme wala mafuta.

“Ukinipa jenereta pia siwezi, sitakuwa na hela ya kununua mafuta kila siku labda nipate njia ambayo hainihitaji hela kila siku, hiyo pia labda nikopeshwe,” amesema Martha huku akiitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TAdB) kuwaangalia mkulima mmoja mmoja.

Hata hivyo, wakati wakizitaka benki kujikita katika ukopeshaji wa mifumo ya umwagiliaji inayotumia jua, tayari zipo taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo hiyo kwa wakulima, wafanyabiashara na hata kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Katika upande wa kusaidia kilimo cha umwagiliaji zipo kampuni mbalimbali ambazo tayari zinatoa mikopo hiyo kwa wakulima ikiwemo Elico foundation, Simusolar, Mysol zinazofanya kazi katika mikoa tofauti nchini ikiwemo Morogoro, Iringa na Dodoma.


Kilichofanyika

Kuhusu mikopo, Bajeti ya Kilimo 2024/2025 iliyoakisi taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwaka 2023 imeonyesha jumla ya mikopo iliyotolewa na taasisi za fedha nchini ni Sh33.159 trilioni ambapo kati ya hiyo Sh3.317 trilioni ilitolewa kwenye Sekta ya Kilimo.

Mikopo hiyo ni sawa na asilimia 10 ya mikopo yote huku miongoni mwa taasisi za fedha zilizotoa mikopo hiyo ni TADB iliyotoa Sh138.119 bilioni, CRDB ilitoa Sh1.41 trilioni, NMB ikitoa Sh1.7 trilioni na kiasi kilichobaki kimetolewa na taasisi nyingine za fedha.

Pia katika kipindi hicho TADB imeongeza taasisi mbili za fedha zinazotumia mfuko wa dhamana ambazo ni Self Micro Finance na Exim Bank Tanzania. Hatua hii imewezesha utoaji wa mikopo yenye thamani ya Sh138.11 bilioni kwenye Sekta ya Kilimo Mazao kwa njia ya moja kwa moja na Sh41.817 bilioni kupitia mfuko wa dhamana ya mikopo kwa wakulima wadogo.

Wakati hili likielezwa pia Serikali imeendelea kujenga skimu za umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini ili hasa katika maeneo ambayo yanafaa.


Ushuhuda kupungua gharama

Katika utafiti ule wa ACME uliangazia baadhi ya vikundi vilivyofanikiwa kupunguza gharama za uzalishaji kupitia umeme jua Tanzania.

Moja ya kikundi ambacho kilihusika katika utafiti huu kikundi cha Jitume kinachomiliki ekari 26 za umwagiliaji zilizopo katika skimu ya Lupembe Lwasenga ambapo wanakikundi walieleza ahueni wanayoiona baada ya kuachana na matumizi ya jenereta katika kazi zao.

Imeelezwa kuwa kikundi hicho sasa kinaokoa Sh70,000 kila siku zilizokuwa zikitumika kununua mafuta.

Kikundi kingine ni cha Pinos Farm kinachomiliki ekari 16 wilayani Iringa kilichokuwa kikitumia Sh50,000 kila siku kwa ununuzi wa mafuta. Vikundi hivyo kwa sasa vinatumia umeme jua katika kilimo cha umwagiliaji kwa msaada wa Taasisi ya Elico.