Wakulima waipongeza Serikali kwa ruzuku ya mbolea

Muktasari:

Baadhi ya wakulima nchini wameishukuru Serikali kwa kuweka ruzuku katika mbolea hali iliyosababisha bei yake kushuka.

Songwe. Baadhi ya wakulima mkoani hapa wameeleza kupokea kwa faraja taarifa ya Serikali kuweka ruzuku kwenye mbolea itakayoshusha bei ya bidhaa hiyo kutoka Sh130, 000 za sasa na kuwa Sh70, 000.

Jana Agosti 8 mwaka huu wakati wa kilele cha maadhimisho ya Nanenane, Waziri wa Kilimo Hussen Bashe amesema mpango wa ruzuku ya mbolea umesaidia kushuka bei, ambapo mbolea ya kupandia (DAP) itauzwa kwa Sh70, 000 na ya kukuzia (Urea) itauzwa Sh70, 000 kutoka Sh124, 734.

Bahati Siwale ambaye ni mkulima mkazi wa Kata ya Kilimampimbi amesema punguzo hilo ni ishahara ya Serikali kuwakumbuka wakulima, kwani walikuwa wameshaanza kukata tamaa kwa upatikanaji wa bidhaa hiyo.

"Msimu uliopita wa mwaka jana wakulima wengi tulipunguza ukubwa wa mashamba na kuamua kulima eneo dog Ili kukidhi mahitaji ya kayak kutokana na bei kuwa juu huku mazao yakiuzwa bei ya chini," amesema.

Naye Gress Mwampashi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiona kero ya wakulima ambayo ilikuwa mzigo mzito wamehitwisha.

"Tunamshukuru Rais kwa kuliona suala la bei ya mbolea, lakini tunamuomba awe makini, kwani wanaweza kunufaika wachache na kuacha watu wa hali ya chini wakiteseka," amesema Mwampashi

Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya wakulima nanenane Jana Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wakati akizundua mpango wa ruzuku ya mbolea aliiagiza Wizara ya Fedha kupeleka fedha haraka ili mpango huo uanze Agosti 15 mwaka huu.