Walalamikia gharama kufunga mifumo ya umeme, Rea yaonesha njia

Mhandisi wa miradi Kanda ya Ziwa kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Ernest Makale (wakwanza kushoto) akionyesha kifaa cha umeme tayari (UMETA) kwa wananchi (hawapo pichani), alichokitaja kuwa kinapunguza gharama za kufunga mfumo wa umeme majumbani. Picha na Samirah Yusuph

Muktasari:

Wamesema wamekuwa wakitozwa kati ya Sh150,000 hadi Sh300,000 kufunga mifumo ya umeme kwenye vyumba viwili bei ambayo baadhi ya mafundi wanadai inatokana na vifaa vya umeme kuwa juu.

Bariadi. Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wamesema gharama za kufunga mifumo ya umeme kwenye nyumba zao zimekuwa kikwazo cha kupata huduma hiyo licha ya Serikali kuweka Sh27,000 ya kuwaunganishia nishati hiyo.

Wamesema wamekuwa wakitozwa kati ya Sh150,000 hadi Sh300,000 kufunga mifumo ya umeme kwenye vyumba viwili bei ambayo baadhi ya mafundi wanadai inatokana na vifaa vya umeme kuwa juu.

“Tunatamani tupate mafundi ambao watakuja na bei elekezi za vifaa ili bei ipungue, kwa sasa kila mmoja anakuja na bei yake jambo ambalo linapunguza hamasa ya kuunganishiwa umeme,”amesema Paulo Shosha mkazi wa kijiji cha Halawa

Akihamasisha wananchi hao kuunganisha huduma za umeme majumbani kupitia mradi wa Rea awamu ya tatu hatua ya pili Julai 20, 2023, Mhandisi wa miradi Kanda ya Ziwa kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Ernest Makale amesema ili kuepusha gharama za ufundi na usumbufu kwa wananchi wanaweza kutumia huduma ya umeme tayari (Umeta) ambayo ina gharama ndogo.

“Umeta gharama yake haizidi 65,000 na inatumika sawa na ukiwa na mfumo wa umeme unaweza kuunganisha vifaa kama kawaida," amesema Makale

Nao baadhi ya mafundi umeme wilayani humo wamesema wingi wa vishoka katika huduma ya kuunganisha mfumo wa umeme majumbani umekuwa kikwazo kwa wananchi kuwa na nishati hiyo.

Wamedai vishoka hao wamekuwa wakiwahi maeneo ya vijijini ambayo yanafikiwa na mradi wa Rea, kuanza kuwalaghai na kuwatoza kiasi kikubwa cha fedha.

“Wanapofika huko wanasema wametoka Tanesco, wananchi wanaamini, wanawapa kazi na ni ukweli kuwa kazi zao hazina ubora na nyingine unaweza kukuta wamefanya nusu haijakamilika na wameondoka hivyo inakuwa ni hasara kwa wananchi,”

“Mafundi tumesajiliwa, tuna leseni, mhuri na majina yapo kwa viongozi wa vijiji hivyo wananchi watumie mafundi hao kwenye maeneo yao kuepusha kutapeliwa,” amesema mmoja wa mafundi hao