Walimu wenye ulemavu wamuomba Spika mambo manne

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akiwa na viongozi wa CWT, Katibu Mkuu, Japhet Mangana (kushoto) na Ulumbi Shani ambaye ni mwenyekiti wa idara ya walimu wenye ulemavu CWT.

Muktasari:

  •  Idara ya walimu wenye ulemavu  ya makao makuu ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) imemuomba Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson asaidie kuwasisistiza waajiri kusoma sheria zinazoongoza vyama vya wafanyakazi kupunguza migogoro mahali pa kazi.

Dodoma. Idara ya walimu wenye ulemavu  ya makao makuu ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), imemuomba Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kusaidia mambo manne ikiwamo kusisitiza Serikali iharakishe  maboresho  ya sera kuhusu wenye ulemavu.


Wametoa maombi hayo jana Januari 31, 2024 walipokutana na Spika, Dk Tulia Ackso walipokwenda kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mabunge Duniani na kuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kushika nafasi hiyo.

Walimu hao wenye ulemavu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara walikuwa takriban 40 wamekutana na Spika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa na kuhudhiriwa na Katibu Mkuu wa CWT, Japhet Maganga.

Hotuba yao iliyosomwa na Mkuu wa Idara ya Walimu wenye ulemavuna wa CWT, Robert Bundala, wamemuomba Dk Ackson asaidie kuieleza Serikali iharakishe maboresho  ya Sera ya Taifa ya huduma na maendeleo ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004.

Pia, wamemuomba asaidie kuileleza Serikali iharakishe kufanya marekebisho machache ya sheria namba 9 ya mwaka 2010, ili iwanufaishe watu wenye ulemavu wakiwemo walimu wenye ulemavu.

Bundala amesema wanaiomba Serikali kupitia Spika itoe kipaumbele kwa walimu wenye ulemavu kuwapatia mafunzo ya mtalaa mpya, ili waweze kutekeleza majukumu yao bila vikwazo sambamba na wenzao wasio na ulemavu.

“Kunapotolewa vitabu vya mtalaa mpya viendane sambamba na vya nukta nundu, ili kuwasaidia walimu na wanafunzi wenye ulemavu kusoma na kufundisha bila utegemezi.

“Sisi walimu wenye ulemavu tunatambua nafasi ya mhimili muhimu wa Bunge unaouongoza katika utungaji wa sheria, kwa hiyo tunakuomba kuwasisistiza waajiri kusoma sheria zinazoongoza vyama vya wafanyakazi kupunguza migogoro mahali pa kazi,” amesema Bundala.

“Miongoni mwa mengi uliyoyafanya na unayoendelea kuyafanya tumeshuhudia katika siku za hivi karibuni ni pamoja na kuikumbusha Serikali inapochukua nafasi ya kushughulikia masuala ya watumishi wa umma wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali kuhukumiwa bila ya kuwapa nafasi ya kusikilizwa, rejea walimu wakuu wawili kutoka halmashauri ya Tunduma mkoani Songwe mwaka 2023. 

“Umekuwa  ukiwakumbusha wafanyakazi walioko  kwenye idara moja inapotokea mgogoro kuna vyama vya wafanyakazi zaidi ya kimoja katika  idara hiyo kuzingatia takwa la kisheria kuhusu ada ya uwakala kwa chama chenye sifa.

“Hasa masuala ya vyama vya wafanyakazi,  kwani ni takwa la kisheria na nchi yetu mara zote inaongozwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Bundala.

Amesema Dk Ackson amekuwa kitoa mchango mubwa katika sekta ya elimu yenye lengo la kuhamasisha ufaulu kwa wanafunzi wakiwemo wenye ulemavu na kutoa motisha kwa shule, wanafunzi na  walimu.

“Idara ya walimu wenye ulemavu inakuomba uendelee na moyo huu na Watanzania wapenda maendeleo wajifunze kwa mifano hai kutoka kwako.

Kwa upande wake, Dk Ackson amekubali ombi lao la kuwa mlezi wao, pia ameeleza kuridhishwa kwake na namna walemavu wanavyojitokeza katika kutetea haki zao na kuwatia moyo.