Walioibiwa mtoto mchanga watamani kukutana na Waziri Mkuu
Mtoto wa siku 42 aliyeibwa.
Muktasari:
- Mtoto huyo aliyekuwa na siku 42, tangu azaliwe, aliibiwa katika Hospitali ya Nguvu Kazi Chanika Julai 6, 2026 alipokuwa amepelekwa kupatiwa chanjo.
Dar es Salaam. Wakati mtoto mchanga aliyeibwa hospitalini Chanika akifikisha siku 23 tangu alipochukuliwa na mtu asiyejulikana, wazazi wake wameomba kukutana na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ili kumwelezea wanayopitia kutokana na tukio hilo.
Mtoto huyo aliyekuwa na siku 42, tangu azaliwe, aliibiwa katika Hospitali ya Nguvu Kazi Chanika, jijini Dar es Salaam Julai 6, 2026 alipokuwa amepelekwa na mama yake kwa ajili ya kupata chanjo.
Katika tukio hilo, mama huyo anayeitwa Sharifa Kassim, aliibiwa mtoto huyo baada ya kumkabidhi kwa dada aliyedhani ni daktari katika hospitali hiyo baada ya kutaka kwenda kujisaidia.
Licha ya kumkabidhi mtoto na pochi yake, baada ya kurudi alikuta tu pochi huku mtoto akiwa kaondoka na dada huyo.
Tangu siku hiyo, walichukua hatua mbalimbali za kumtafuta mtoto huyo bila mafanikio.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Julai 28, 2026, baba wa mtoto huyo, Taliq Abdallah, amesema mpaka sasa zimepita siku 23 tangu kutokea kwa tukio hilo, bado wapo katika huzuni na kutojua mtoto wao yupo wapi na je, huko alipo ni mzima au la.
Abdallah ameeleza kinachomuumiza zaidi ni namna jambo hilo linavyoshughulikiwa na kueleza kuwa hawaridhiki na ndio maana wanatamani kuonana na Waziri Mkuu ili wamwambie wanayoyapitia labda huenda akawaelewa.
“Kutokana na namna jambo linavyoshughulikiwa, siridhiki kwa kweli, yaani natamani kokote nitakaposikia Waziri Mkuu yupo niende kukutana naye nimuelezee kuhusu jambo hili labda huenda akawasukuma zaidi watendaji wake kulifanyia kazi,” amesema Abdallah.
Amesema kwa muda ambao muhusika aliyeiba mtoto na picha yake ilipotangazwa alitegemea angepatikana kwa urahisi lakini haijawa hivyo.
“Yaani dada yangu hata hiyo picha yenyewe hadi huyo dada anayetuhumiwa kuiba mtoto kuwekwa hadharani tulifanya kazi kweli kuipata na hii ni baada ya kuona ukimya umetawala tukaamua kwenda kwa viongozi ngazi ya Wilaya.
“Tunaamini kumtafuta mtu anayejulikana ni rahisi kuliko asiyejulikana, kwa kuwa sura yake imeonekana.
“Lakini hatujui shida nini, ndio maana tunaona bora tuende ngazi za juu kwa kuwa huku chini suala hilo linaenda taratibu huku wazazi tukiendelea kuugulia maumivu yasiyo na mfano,” amesema Abdallah.
Wakati Abdallah akizungumza hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema bado wanaendelea na uchunguzi.
Kuhusu malalamiko ya wazazi hao kufanyika kwa jambo hilo taratibu, Kamanda Muliro amesema hata suala la kutangazwa kwa mtuhumiwa mtandaoni ni kazi ya jeshi hilo pia, na huko walipokwenda kulalamika kiongozi wake ni mmoja wa watu walio katika kamati ya ulinzi na usalama wa kanda hiyo.