Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafamilia wanne wafariki dunia baada ya kunywa dawa ya kienyeji, mmoja ashikiliwa

Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa akizungumzia vifo vya watu wanne wa familia moja waliofariki kwa kunywa dawa ta kienyeji.

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Beatrice Urassa (59), kwa tuhuma za kuhusika na vifo vya watu wanne wa familia moja baada ya kuwapa dawa ya kienyeji inayodaiwa kusababisha vifo vyao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha leo Julai 9, 2026 kutokea kwa tukio hilo katika Kitongoji cha Kinyaro, Kata ya Mnadani, Wilaya ya Hai.

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa anadaiwa kuwapatia dawa ya kienyeji watu hao Julai 5, 2026, kabla ya hali zao kuzorota na baadaye kufariki dunia walipokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Machame na Hospitali ya Wilaya ya Hai.

Kamanda Maigwa amewataja waliofariki dunia kuwa ni Hamida Kweka (26), Robson Meena (34), Ismail Uronu (34) na Kamama Uronu (45).

"Ni kweli kwamba Julai 5, 2026, katika Kitongoji cha Kinyaro, Kata ya Mnadani, Wilaya ya Hai, watu wanne wa familia moja walifariki dunia baada ya kunywa dawa ya kienyeji."

“Walifariki wakiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Machame na Hospitali ya Wilaya ya Hai," amesema.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa anadaiwa kuwapatia dawa hiyo ya kienyeji watu hao, huku chanzo na mazingira ya tukio hilo yakiendelea kuchunguzwa.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hili. Uchunguzi utakapokamilika, hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa," amesema Kamanda Maigwa.