Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wawili wafariki dunia wakinywa dawa kujikinga na magonjwa ya kishirikina

Muktasari:

  • Ni baada ya kunyeshwa dawa ya kienyeji  na baba yao kwa lengo la kuwakinga na magonjwa yatokanayo na imani za kishirikina kwa kile kilichoelezwa walikuwa wakiugua kwa kipindi kirefu maradhi ya tumbo na vichomi.

Mbeya. Watu wawili wa familia moja wamepoteza maisha na wengine watatu kunusurika na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya baada ya kunyweshwa madawa ya kienyeji.

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga ameliambia Mwananchi Digital  leo  Jumatano, Februari 22, 2023 huku akibainisha kumshikilia baba wa familia hiyo, Makeremo Nyasa (57) mkazi wa Kitongoji cha Kitete, Kata ya Bwawani wilayani humo.

Kamanda Kuzaga amesema tukio hilo limetokea Februari 19 mwaka huu saa 2.00 asubuhi na kuwataja waliopoteza maisha kuwa ni Raphael Makeremo (26) na Mafunda Makeremo (18).

Aidha amewataka walionusurika baada ya kukimbizwa katika Hosptali ya Wilaya ya Chunya kwa matibabu kuwa ni, Nchambi  Lusangija (50) Manyirizu Kulyehelwa (7) na Njile Makeremo (18).

Kamanda Kuzaga amesema kuwa chanzo cha tukio hilo ni baada ya mtuhumiwa kuona watoto wake wamekuwa wakiugua muda mrefu maradhi ya tumbo na vichomi ndipo akahusishwa magonjwa hayo yanatokana na imani za kishirikina.

Amesema kutokana na kuwa na imani hiyo ndipo alikwenda kwa mganga wa kienyeji maarufu kama “Gwalinzi” mkazi wa  Kijiji cha Goririma, Kata ya Lupa kuchukua dawa na kuwanywesha wanafamilia kwa lengo la kuwakinga na magonjwa yatokanayo na imani za kishirikina.

Kuzaga amesema kuwa baada ya kutokea vifo hivyo mganga huyo amekimbia kusikojulikana na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka, huku mtuhumiwa anayeshikiliwa akiendelea kuhojiwa zaidi kuhusiana na tukio hilo.

Kamanda  Kuzaga ametoa  wito kwa jamii kuachana na imani potofu za kishirikina kwani zinasababisha madhara makubwa na badala yake watafute tiba ya maradhi yanayowasumbua kwa kwenda hospitali kwa ajili ya vipimo na matibabu toka kwa matabibu.

“Nionye waganga wapiga ramli ambao mnaendesha shughuli zenu bila vibali na kutambulika kisheria kuacha mara moja kwani Jeshi la Polisi halitawavumilia litawasaka na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sharia,” amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya mkoani hapa, Saimon Mayeka amelaani kitendo hicho na kwamba tayari ametoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha mganga huyo anakamatwa na kuchukuliwa hatua.

“Nitoe wito kwa wananchi kuepukana na tabia ya kuamini waganga wa tiba za asili ambao hawatambuliwi kisheria na badala yake wafike kwa watabibu kwenye hosptali na vituo vya afya,” amesema.

Mkazi wa kibaoni wilayani humo, John Saimon ameomba Serikali kupiga marufuku waganga wapiga ramli chonganishi kwani wamekuwa ni sababu kubwa ya migogoro ya kifamilia na kuchochea matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto.