Wanafunzi 15 St Mary Goreti walazwa KCMC wakiugua tumbo
Muktasari:
- Wanafunzi hao walifikishwa hospitalini hapo jana Machi 6, 2024 wakikabiliwa na changamoto hiyo na tayari wameanza kufanyiwa kipimo cha 'culture'.
Moshi. Wanafunzi 15 wanaosoma shule ya sekondari St. Mary Goreti iliyopo manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) wakikabiliwa na ugonjwa wa matumbo.
Wanafunzi hao wamefikishwa hospitalini hapo jana, Machi 6, 2024 na tayari wameanza kufanyiwa kipimo cha ‘culture’ (kuotesha vimelea kubaini ugonjwa) na wanaendelea na matibabu ya awali, huku afya zikiendelea kuimarika.
Akithibitisha kulazwa kwa wanafunzi hao, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo amesema walifikishwa hospitalini hapo wakikabiliwa na homa ya matumbo na tayari wamechukuliwa vipimo, ili kubaini ni ugonjwa gani.
“Hawa wanafunzi waliletwa hapa kwetu KCMC, walikuwa na changamoto ya kuumwa ugonjwa wa matumbo, wamechukuliwa kipimo cha culture na majibu bado hayajatoka, yatakapotoka ndio tutajua wanaumwa ugonjwa gani,” amesema.
Kwa upande wake, mganga mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Dk Jairy Khanga amethibitisha kulazwa kwa wanafunzi hao katika hospitali ya KCMC na kueleza kwa sasa vipimo vimepelekwa maabara, ili kufanyiwa uchunguzi kubaini tatizo ni nini.
“Taarifa nilizonazo ni kwamba kuna watoto wa St Maria Goreti wamepata shida na wako KCMC, jana walipelekwa 11 na leo wamepelekwa wanne, hivyo jumla ni 15. Kwa sasa vipimo vimepelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi, tusubiri majibu,” amesema Khanga.
Mmoja wa watawa aliyejitambulisha kama kaimu mkuu wa shule hiyo kwa sharti la kutotaka kutajwa jina lake, amesema hawezi kuzungumza chochote kuhusiana na suala hilo na kwamba msemaji ni mganga mkuu wa manispaa ya Moshi.
“Kuhusu watoto kulazwa hospitali hatuwezi kuzungumza lolote, wasilianeni na mganga mkuu wa manispaa wao wataweza kutoa taarifa,” amesema mtawa huyo.