Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi Visiga Sekondari wapatiwa baiskeli kupunguza changamoto ya usafiri

Msimamizi wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja kutoka Halotel, Hanh Thi hong Nguyen alimkabidhi baiskeli, Mkuu wa Sekondari ya Visiga, Aurelian Njau (aliyevaa suti nyeusi) kwa baadhi ya wanafunzi wanaokaa mbali na shule hiyo ili wazitumie kwa ajili ya usafiri. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Shule ya Sekondari Visiga ina jumla ya wanafunzi 1337 lakini wanafunzi zaidi 70 wanatumia muda mrefu kutembea kwa miguu kutoka majumbani kwako hadi shuleni.

Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Visiga, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, sasa wataondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni baada ya kupatiwa msaada wa baiskeli.

Wanafunzi hao, ambao wamekuwa wakitumia hadi masaa matatu kutembea kwa miguu kwenda shuleni, wamesema hali hiyo imekuwa ikiathiri mahudhurio yao darasani, hasa nyakati za asubuhi. Aidha, wasiwasi umetolewa kuwa wanafunzi wa kike wako hatarini kujiingiza katika vishawishi kutokana na changamoto hiyo ya usafiri.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada wa baiskeli 20 kutoka Kampuni ya Halotel, Mkuu wa Shule hiyo, Aurelian Njau amesema baiskeli hizo zitawanufaisha wanafunzi wanaotoka vijiji vya mbali kama Saini, Madabala na Matuga.

"Wanafunzi hawa wanatumia muda wa masaa mawili na nusu hadi matatu kwenda na kurudi nyumbani. Hali hii huathiri muda wao wa kujifunza, hivyo kama shule tumekuwa tukiwapa muda wa ziada wa kusoma ili kuwasaidia kuendana na wenzao," amesema Njau.

Aliongeza kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,337 wa kidato cha kwanza hadi cha nne, ikiwa na madarasa 23, madawati zaidi ya 1,000 na walimu 53. Hata hivyo, changamoto kubwa ni wanafunzi zaidi ya 70 wanaotembea umbali mrefu kufika shuleni.

Diwani wa Kata ya Visiga, Mbegu Legeza, ameishukuru Halotel kwa msaada huo na kusisitiza umuhimu wa elimu kama urithi bora kwa watoto. Hata hivyo, alitaja changamoto zinazokabili shule hiyo kuwa ni uhaba wa madarasa, madarasa 10 yaliyopo kuwa chakavu, upungufu wa walimu na hitaji la mabweni kwa wanafunzi wanaoishi mbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara wa Halotel, Abdallah Salum, amesema kampuni hiyo iliguswa na changamoto wanayopitia wanafunzi hao na kuona umuhimu wa kusaidia.

"Katika kuunga mkono juhudi za Serikali, tumeamua kutoa baiskeli hizi ili kuwasaidia wanafunzi hawa kupunguza changamoto ya usafiri," amesema Salum.

Ezuna Ramadhani na Simon Michael, wanafunzi wa kidato cha pili walionufaika na msaada huo, walisema baiskeli hizo zitawasaidia kuwahi vipindi na kurudi nyumbani mapema, hivyo kuongeza ufaulu wao. Walipendekeza pia kujengewa mabweni ili kuondoa kabisa changamoto ya usafiri.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Visiga, Ibrahim Mpati, amewataka wanafunzi na wazazi kuzitunza baiskeli hizo ili zidumu kwa muda mrefu.

Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Mawasiliano wa Halotel, Roxana Kadio, amesema huu ni mwanzo wa ushirikiano kati ya kampuni hiyo na shule hiyo, na kwamba wataendelea kutoa msaada zaidi kwa wanafunzi ili kuwawezesha kupata elimu bila vikwazo.