Wanafunzi waliofariki kwa kuangukiwa na gema wazikwa

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akitoa salamu za pole kwa  familia iliyopoteza watoto wawili kwa kudondokewa na gema la udongo wakati wakiwa wamelala nyumbani kwao.

Muktasari:

Wanafunzi hao wa familia moja, waliangukiwa na gema la udongo kwenye nyumba waliyokuwa wamelala usiku wa kuamkia jana, Januari 31 kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.

Same. Wanafunzi hao waliofariki kwa kuangukiwa na gema la udongo wakiwa wamelala, wamezikwa leo katika makaburi ya familia yaliyopo katika kijiji cha Kambeni wilayani ya Same Mkoa wa  Kilimanjaro.

Wanafunzi hao  Rahel Elineema (13), mwanafunzi wa kidato cha kwanza, shule ya Sekondari Myamba na Selina Elineema (7) mwanafunzi wa darasa la pili, shule ya msingi Kambeni wilayani humo, wamezikwa leo katika makaburi ya familia yaliyopo katika kijiji cha Kambeni.

Wanafunzi hao wa familia moja, waliangukiwa na gema la udongo kwenye nyumba waliyokuwa wamelala usiku wa kuamkia jana, Januari 31 kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.

Jana Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alithibitisha kutokea kwa vifo vya wanafunzi hao ambapo amesema walifariki dunia baada ya nyumba waliyokuwa wamelala kuangukiwa na gema la udongo.

Alisema kutokana na mvua nyingi zinaendelea kunyesha maeneo ya milimani wilayani humo, hali ni mbaya kutokana na kuharibika kwa miundo mbinu ya barabara na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuchukua tahadhari wakati wa kipindi hiki ambacho mvua ni nyingi.

Akizungumza leo,  katika ibada ya mazishi ya wanafunzi hao, Mkuu wa wilaya ya Same, Kaslida Mgeni ametoa pole kwa famlia hiyo kwa kupoteza watoto wawili kwa mpigo,  ambapo amesema mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo hazijaleta madhara kwa binadamu pekee na kwamba zaidi ya ekari 800 za mpunga zimesombwa na maji.

"Mvua hizi zilizonyesha sio tuu zilipoteza maisha ya watu lakini pia zaidi ya ekari 800 za mpunga wilayani kwetu zimeondoka na maji, lakini barabara zimekatika na kuharibka, Serikali inaendelea kuhakikisha miundombinu inarudii ili maisha yaendelee," amesema DC Mgeni.

Januari 10, mwaka huu, watu watatu wilayani  humo walifariki dunia kutokana na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha wilayani humo.