Wanafunzi watengeneza taulo za kike Karatu
Baadhi ya wanafunzi waliojengewa uwezo wakutengeneza taulo za kike
Muktasari:
Zaidi ya wanafunzi 3033 wa Tarafa ya Endabash wilayani Karatu mkoani Arusha wajengewa uwezo wa kutengeneza taulo za kike zitakazowasaidia wanafunzi wa kike wanapokuwa katika siku zao za hedhi ili kupunguza utoro shuleni.
Karatu. Zaidi ya wanafunzi 3033 wa Tarafa ya Endabash wilayani Karatu mkoani Arusha wajengewa uwezo wa kutengeneza taulo za kike zitakazowasaidia wanafunzi wa kike wanapokuwa katika siku zao za hedhi ili kupunguza utoro shuleni.
Awali wakizungumzia changamoto ya ukosefu wa taulo za kike za uhakika, baadhi ya wanafunzi wa kike waliopatiwa ujuzi huo walisema walikuwa wanakosa ujasiri kusoma kwa kujiamini kutokana na vifaa walivyokuwa wanatumia kuhofu kudondoka.
Elizabeth Simon amesema walikuwa wanashindwa kuhudhuria masomo kwa siku nne hadi tano wakiwa katika siku zao za hedhi kutokana na miundombinu isiyorafiki kwao ikiwemo sehemu ya kubadilishia taulo.
"Lakini sasa tunawashukuru serikali kwa kushirikiana na shirika la World vision Tanzania wameweza kutupatia elimu ya utengenezaji taulo za kike na namna ya kuzihifadhi na zinadumu kwa muda mrefu hivyo sasa hivi tunahudhuria masomo kwa muda wote,"amesema Elizabeth.
Kwa upande wake ofisa elimu wa kata ya Buger, Remtula Mollel amesema utoro uliongezeka kwa wanafunzi wa kike kuanzia asilimia 50 kushuka chini hali ilitokana na imani potofu katika jamii kuwa mtoto anapokuwa katika siku zake za hedhi kutoruhusiwa kutembea.
"Imani hizo potofu husababishwa na baadhi ya makabila kutoruhusu mtoto wa kike kuonana na watu anapokuwa katika siku zake za hedhi lakini baada ya shirika la World Vision Tanzania kufika katika ngazi ya jamii kufika nyumba hadi nyumba watoto wa kike wamebadilika,"amesema.
Aidha amesema mahudhurio ya wanafunzi shuleni yameongezeka kwa asilimia 100 kutokana na elimu waliyopatiwa sasa hivi wametambua usalama wa hedhi hali iliyowapa kujiamini.
Mratibu wa mradi wa Endabash AP, Denis Kikwe amesema wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa wavulana na wasichana wapatao 5835 juu ya afya ya usafi wa hedhi kwani elimu hiyo imesaidia kupunguza utoro pamoja na kuongeza hali wanafunzi wa kike kushiriki shughuli za shule kama michezo.
Pia amesema wamejenga vyoo 31 vyenye huduma jumuishi kwa watoto wenye ulemavu vya wasichana na wavulana ambavyo vimezingatia faragha katika sehemu ya kubadilishia taulo za kike.