Wananchi Kusini wasisitiza haja ya kuwa na Katiba mpya

Wananchi wa Lindi na Mtwara, wakiwa katika mkutano wa kutoa maoni kwenye jukwaa la katiba. Picha Bahati Mwatesa.
Muktasari:
- Maoni hayo yametolewa leo Agosti 22, 2024 kwenye kongamano hilo lililowakutanisha pamoja zaidi ya wadau 200 kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara wakijadili kuhusu mustakabali wa Katiba mpya.
Lindi. Washiriki wa kongamano la Jukwaa la Katiba kutoka mikoa ya Kusini, wametaka mwendelezo wa mchakato wa Katiba mpya ambayo itampunguzia Rais majukumu tofauti na iliyopo sasa inayompa majukumu mengi.
Maoni hayo yametolewa leo Agosti 22, 2024 kwenye kongamano hilo lililowakutanisha pamoja zaidi ya wadau 200 kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara wakijadili kuhusu mustakabali wa Katiba mpya.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, dereva bodaboda katika manispaa ya Lindi, Hamis Hassan manispaa amesema kuna haja ya mabadiliko ya Katiba ili kuendana na wakati pamoja na kuongeza tija kwa wananchi tofauti na iliyopo sasa ambayo inawanufaisha wachache hasa viongozi.
“Katiba inatakiwa kubadilishwa kwani Rais amepewa mamlaka makubwa sana na pia hii Katiba ya sasa haimnufaishi mtu wa chini, inawanufaisha viongozi, sisi watu wa chini hatunufaiki nayo kabisa,” amesema Hassan.
Kwa upande wake, mkazi wa Mtwara, Shakira Fatawi amesema hivi sasa mambo mengi yamebadilika, Serikali inatakiwa kuona haja ya kubadilisha Katiba, kwani kuna vitu ambavyo vinatakiwa kubadilishwa na sio kuendelea kuwepo hadi sasa.
“Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba ilikuwa nzuri, kama Serikali itakubali ipitishwe kuwa Katiba, vitu vingi vilivyomo vinaweza kubadilishwa na hata mtu wa chini akanufaika nayo tofauti na hii tunayotumia,” amesema Fatawi.
Mkuu wa programu ya Jukwaa la Katiba Tanzania, Thobiasi Nyaisanga amesema kwenye Katiba iliyopo sasa ina upungufu ambao unatakiwa kurekebishwa kwa kuchukua maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi na kwenda kuyafanyia kazi na kuweza kupata Katiba bora.
“Tumeona tuwakutanishe watu kutoka Lindi na Mtwara katika kukusanya maoni ili yafanyiwe kazi na kupata Katiba nzuri,” amesema Nyaisanga.
Hata hivyo, Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Lindi wa CCM, Patric Magarinja amesema dhamira kubwa ya chama hicho ni kuwa na Katiba mpya ili kutoka tulipo.
“Sisi kama Chama cha Mapinduzi, dhamira yetu ni kuwa na Katiba mpya ili tutoke tulipo, na ndiyo maana kwa mkoa wetu wa Lindi tumekuwa tukitekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo ipasavyo ili kufika pale Rais Samia anataka tufike,” amesema Mgarinja.