Wananchi Rombo waomba kupimiwa ardhi

Muktasari:

  • Wananchi wa Kata ya Tarakea Motamburu, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wameiomba serikali kuharakisha urasimishaji wa maeneo yao ili kupunguza migogoro ya mipaka ambayo imekuwa ikiwatesa kwa miaka mingi.


Rombo. Wananchi wa Kata ya Tarakea Motamburu, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wameiomba serikali kuharakisha urasimishaji wa maeneo yao ili kupunguza migogoro ya mipaka ambayo imekuwa ikiwatesa kwa miaka mingi.

Wamesema serikali kutowapimia maeneo yao imekuwa ikiruhusu ujenzi holela na wakati mwingine wananchi kufungiana njia za kuingia kwenye makazi hayo.

Wameyasema hayo Oktoba 5, 2022  katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Motamburu wilayani humo, wakisema wako tayari na watawapa ushirikiano wataalam wa ardhi watakapofika kwenye maeneo yao  ili kukamilisha shughuli hiyo ya urasimishaji wa maeneo.

Mmoja wa wakazi hao, Gasper Kimario amesema suala la kupima ardhi na kuweka mipaka kwenye maeneo ya wananchi litapunguza migogoro isiyo ya lazima kwenye makazi ya wananchi na kwamba litaufanya mji wa Tarakea kuwa na maendeleo makubwa.

"Suala la kupima ardhi na kurasimisha maeneo ya wananchi ni jambo jema na inaleta faida nyingi hasa katika mji huu wa Tarakea ambao unakuwa kwa kasi, maeneo mengi yatakuwa na thamani na kuchochea maendeleo kwenye mji huu na kwa wananchi kwa ujumla.

"Kupimwa kwa mji wetu wa Tarakea manufaa yatakuwa ni mengi, tutaona mji wetu wa Tarakea ukipangika vizuri kwasababu sisi tumejiandaa kwasababu tumeona jinsi watu wanavyojijengea kiholela na kusababisha migogoro isiyoisha kila siku, tunaishukuru serikali maana tunajua hili litatekelezwa kwa wakati na kwa haraka".

Kwa upande wake Grace Tarimo, Mkazi wa kijiji cha Mbomai alisema suala la upimaji wa ardhi ni muhimu kwa kuwa wananchi wamekuwa wakijenga ujenzi holalea na kusababisha migogoro ambayo imekuwa ikipelekea watu kujeruhiana.

"Suala la upimaji wa ardhi ni muhimu maana watu wamekuwa wakijenga bila utaratibu na  njia za kwenda kwenye makazi ya watu hazipo,  hata moto ukitokea hakuna sehemu ya gari kupita maana nyumba zimejengwa bila utaratibu," amesema.

Naye diwani wa kata hiyo, Felichism Oisso amesema zipo barabara na mitaa ambayo tangu mwaka 1992 hazijafunguliwa na ujenzi holela unaendelea ambapo baadaye inaweza kuja kuwasabishia wananchi hasara pale nyumba zao zitakapovunjwa kupisha barabara, hivyo anaiomba serikali kuharakisha maeneo hayo kupimwa ili kuondoa adha hiyo na hasara ambayo wananchi watakumbana nayo.

"Tusipopima haya maeneo sasahivi tutasababisha hasara kubwa kwa wananchi wetu, kuna barabara na mitaa tangu mwaka 1992 zinapaswa zifunguliwe lakini bado wananchi wanajenga kiholela katika maeneo hayo alafu baadaye tutaanza kuvunja na kuwaletea wananchi wetu hasara," amesema.