Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi wahimizwa kutumia mfumo kuwatambua mawakili feki

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Seif Kulita akizungumza na waandishi wa habari mkoani Shinyanga.

Muktasari:

  • Mahakama Kuu imekuja na mfumo wa kielektroniki e-Wakili, ukiweka jina la wakili, mfumo utatambua kama anaruhusiwa kuhudumia wananchi kama wakili au haruhusiwi.

Shinyanga. Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Asha Mwetindwa amesema Mahakama imekuja na mfumo wa kielektroniki wa e-Wakili ili kuwatambua mawakili wanaotakiwa kufanya kazi hiyo, hivyo amewasihi wananchi kuutumia.

Amesema mfumo huo, ambao una miaka mitatu sasa tangu kuanzishwa kwake, bado haujajulikana kwa wananchi, jambo linaloweza kuwasababishia usumbufu endapo watamtumia wakili ambaye hatambuliwi.

Mwetindwa amebainisha hayo leo, Mei 24, 2025, wakati akizungumza na vyombo vya habari katika mafunzo yaliyofanyika Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga iliyopo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga.

 “Kuna mawakili ambao hawaruhusiwi kumwakilisha mwananchi mahakamani, inaweza kuwa hana leseni au leseni anayo lakini imeisha muda wake, huyo haruhusiwi na tunaweza kumtambua kupitia mfumo wa e-Wakili ambapo ukiingiza jina, mfumo unaonyesha kama anaruhusiwa, haruhusiwi au hatambuliki kabisa,” amesema Mwetindwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Gerard Chami amesema kama mwananchi anaona haridhishwi na mapokezi ya Mahakama alizopita, anaruhusiwa kuwasiliana moja kwa moja na makao makuu.

“Kupitia Call Center 0800750247, akipiga, mazungumzo yanahifadhiwa moja kwa moja na kutoka makao makuu. Viongozi wa Mahakama wanaweza kuchukua na kusikiliza au kumsikiliza moja kwa moja mwananchi anapozungumza.

“Hii inafanya utendaji kazi kuwa mzuri na kusimamia haki. Nawaomba waandishi wa habari, namba hii iwafikie wananchi,” amesema Chami wakati akizungumzia namna wanavyowasaidia wananchi wenye changamoto za kisheria.

Aidha, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Seif Kulita amesema atafanya vikao na mahakimu wa Mahakama za wilaya na hakimu mkazi ili kujadili namna ya kushirikiana na vyombo vya habari.

“Kuna malalamiko kuhusiana na mahakimu wa Mahakama za wilaya na hakimu mkazi kutoonyesha ushirikiano kwa waandishi wa habari. Hili nitazungumza nao, hasa katika kutoa taarifa muhimu ambazo haziharibu kazi za Mahakama,” amesema Jaji Kulita.