Wananchi watoa ekari 25 kujenga sekondari ya wasichana

Eneo la mradi inapojengwa shule ya wasichana ya sayansi Mkoa wa Katavi iliyopo Kijiji cha Songambele. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

  • Wakazi Kijiji Songambele wajitolea ekari 25 bure zijengwe shule maalumu ya sayansi ya wasichana ya mkoa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na juhuzi zake za kuboresha elimu nchini.

Katavi. Ni katika hatua ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu, wakazi wa Kijiji cha Songambele, Halmashauri ya Nsimbo, mkoani Katavi, wametoka eneo la ekari 25, kwa ajili ya ujenzi wa sekondari maalum ya Sayansi kwa wasichana itakayogharimu Sh4 bilioni.

Mradi wa ujenzi wa shule hiyo umeanza kutekelezwa, ambapo tayari upo katika hatua ya msingi, unatarajiwa kuwa na majengo 23, na ni kwaajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita ndani na nje ya mkoa, huku ukitarajiwa kukamilika ndani ya siku 90.

Kwa niaba ya wananchi hao, leo Septemba 14, 2023; Mwenyekiti wa Serikali ya hicho, Enock Kapela amesema baada ya kupata taarifa za ujio wa mradi huo, kwa pamoja waliguswa na kuamua kutoa ardhi hiyo.

“Ametufanyia jambo njema sana Rais Samia, tupo tayari kushirikiana pamoja hadi mradi huu utakapokamilika, wapo waliotoa ekari tano, mbili na zaidi,” amesema mwenyekiti huyo na kuongeza;

“Tunamuomba mama yetu aendelee kutuletea miradi mingine, shule hii ina manufaa kwetu na mikoa mingine, watoto wetu watakuja kusoma hapa,” amesema Kapela.

Kwa upande wake Diwani Viti Maalumu Kata ya Mtapenda, Gerimana Mwanandota, amesema shule hiyo itapunguza gharama kwa wazazi kuwasafirisha watoto wao wanaofaulu na kupangiwa kwenda kusoma nje ya mkoa.

“Itasidia wazazi walio na maisha duni kwa sababu gharama zitapungua na watapata fursa ya kufuatilia mienendo ya watoto wao shuleni,” amesema Gerimana.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Nsimbo, Oliver Matelya amesema shule hiyo itakuwa na mabweni 8 yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 80 kila moja.

“Ina vyumba vya madarasa sita, maabara ya Fizikia, Jiografia, Kemia, Bailojia, nyumba za walimu na majengo mengine, hadi sasa tumishajenga msingi kwa majengo 20,” amesema.

Amesema wapo hatua hiyo kutokana na changamoto ya ukosefu wa maji ambapo inawalazimu kuyanunua kutoka umbali mrefu.

“Barabara katika eneo la ujenzi ni mbovu haipitiki kwa urahisi hususani kwa magari yanayobeba saruji na hakuna fedha za usimamizi,” amesema Matelya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nsimbo, Mohamed Ramadhan amesema tayari wamepokea Sh3 bilioni awamu ya kwanza na amezitafutia ufumbuzi changamoto zinazokabili mradi huo.

“Umeme haukuwepo nilitoa taarifa Tanesco wamekuja wapo kazini, maji tumeweka kisima cha muda kipo mita 400 hakikidhi mahitaji, Ruwasa kutoka Ziwa Tanganyika na Kigoma wamefika kuhakiki, Tarura wanashughulikia barabara,” amesema Ramadhan.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, katika ziara yake ya ukaguzi miradi ameiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) mkoa, kuhakikisha wanadhibiti vitendo vya rushwa katika mradi huo.

“Kutokana na ukubwa wa mradi huu na thamani yake Kamanda Takukuru usisubiri kuja kupambana na rushwa zuia kabla rushwa haijatokea,” amesema Mrindoko na kuongeza;

“Tengeneza utaratibu wa usimamizi utakaohakikisha hakuna jambo la ubadhirifu, ukinusa chukua hatua haraka, ofisi ya mkoa itafanya ziara za kushtukiza kila mara sitakubali kumuagusha Rais.”