Wananchi watolewa hofu ujenzi sekondari ya kata

Muktasari:
Kata ya Nyampulukano ni miongoni mwa kata 26 zinazounda Jimbo la Serengerema lililopo mkoani Mwanza ambayo ndiyo kata pekee hisiyo na sekondari.
Sengerema. Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu amewatoa hofu wananchi wa Kata ya Nyampulukano kuwa Sh600 milioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata hiyo haitohamishiwa kwenye kata nyingine kama taarifa za kuhamishwa fedha hizo zinavyosema.
Taarifa zilizosambaa kwa wananchi zilidai kuwa fedha hizo zitahamishiwa Kata ya Mishine kwakuwa Kata ya Nyampulukano haina eneo la kujenga shule hiyo ambazo si zakweli.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Aprili 30, 2023, Tabasamu amesema wananchi walimtuhumu Diwani wa kata hiyo, Amri Kahongo kuhusika kuhamisha fedha hizo zikajenge shule mpya kata ya Mishine badala ya kata yake.
“Shule hii itajengwa Kata ya Nyampulukano eneo lipo Mtaa wa Igogo, itajengwa hapo na siyo sehemu nyingine wananyampulukano nao wapate shule,”amesema Tabasamu
Aprili 25 mwaka huu kwenye mkutano wa hadhara wa mbunge huyo uliofanyika kata ya Nyampulukano ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi, walimtuhumu diwani huyo kuhamisha fedha hizo.
Akizungumzia tuhuma hizo, Diwani wa Kata ya Nyampulukano, Amri Kahogo amesema hakuwa na mamlaka ya kuhamisha fedha hizo bali vikao vilikaa na kufanya maamuzi hayo.
Mmoja wa wananchi wa kata hiyo, Emmanuel Munwas amempongeza mbunge huyo kuhakikisha fesha hizo zinatumika kama zilivyokusudiwa.