Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaodaiwa kuiba mafuta ghafi, upelelezi wao upo mbioni kukamilika

Muktasari:

  • Wanadaiwa kutenda makosa yao, kati ya Juni 2, 2026 na Juni 4, 2026, Mtaa wa Moringe, Wilaya ya Temeke, ambapo wanadaiwa kuiba lita 2800 za mafuta ghafi yenye thamani ya Sh26milioni, mali ya kampuni hiyo.

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya wizi wa lita 2,800 za mafuta ghafi inayomkabili msimamizi wa tanki la mafuta, Kassim Kongwa (43) na wenzake sita, upo hatua za mwisho kukamilika.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne, Juni 30, 2026, wakati shauri hilo lilipotajwa.

Mbali na Kongwa, washtakiwa wengine ni Hemed Abdallah(30), ambaye ni kibarua wa Kampuni ya Azania, Hassan Kimoge(42), Juma Issah(43), Halfan Halfan maarufu kama Ruba, Maria Gulaba ambaye ni opereta wa kiwanda hicho pamoja na mlinzi, Jafar Molel.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na wizi wa lita 2,800 za mafuta ghafi, yenye thamani ya Sh26 milioni, mali ya kampuni ya Mikoani Edible Oil and Detergents Limited.

Winiwa ametoa taarifa hiyo mbele yaHakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Anna Magutu, ambapo alidai kutokana na hali hiyo, anaomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuangalia iwapo upelelezi umekamilika.

Pia, wakili Kasala aliomba Mahakama itoe hati ya wito wa kuwaita washtakiwa waletwe mahakamani wakitokea gerezani, kutokana na leo washtakiwa kutokuletwa.

Hakimu Magutu alikubaliana na ombi hilo na kutoa hati ya kuwaleta washtakiwa mahakamani.

Baada ya kusikiliza hoja za upande wa Jamhuri, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 14, 2026 itakapotajwa.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Juni 16, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 13513 ya mwaka 2026.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa, kati ya Juni 2, 2026 na Juni 4, 2026, katika Jiji la Dar es Salaam, kwa nia ovu, washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu na kuiba mafuta ghafi mali ya kampuni hiyo.

Shtaka la pili ni wizi, ambapo Juni 4, 2026 mtaa wa Moringe, Wilaya ya Temeke, ambapo watuhumiwa hao waliiba lita 2,800 za mafuta ghafi yenye thamani ya Sh26 milioni, mali ya kampuni hiyo.

Shtaka la tatu ni kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote, ambapo katika tarehe hizo na eneo hilo walijipatia lita 2,800 za mafuta wakijua mafuta hayo yalitokana na kosa tangulizi la wizi.