Wanaotoa huduma za ‘massage’ watakiwa kujisajili

Muktasari:

  •  Baraza la tiba asili na tiba mbadala ndio baraza lenye mamlaka ya usajili na utoaji leseni kwa watoaji wa tiba hizo. Watoa huduma za massage wamepewa muda hadi Machi 31 mwaka huu wawe wamejisajili katika Baraza hilo.

Dar es Salaam. Baraza la tiba asili na tiba mbadala Tanzania limeagiza vituo vyote vinavyotoa huduma za kusinga maarufu kama “massage” kuhakikisha vinajisajili pamoja na kusajili watoa huduma wao kabla ya Machi 31 mwaka huu.

Baraza limeeleza kwamba usajili huo utafanyika kwa kituo husika pamoja na watoa huduma hiyo pia wanatakiwa kuwa na vibali kutoka katika baraza hilo. 

Hayo yamebainishwa leo Januari 14, 2022 jijini Dar es Salaam na Ndahali Msigwa kutoka sekretariet ya tiba asili na mbadala wakati akifafanua jambo katika kikao cha bodi kilichowakutanisha kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali kuhusu sekta hiyo.

“Tumetoa muda hadi kufikia Machi 31. Huduma za massage ni tiba mbadala ambayo mtoa huduma anatakiwa kuwa amepata mafunzo maalum, hivyo lazima asajiliwe kabla ya kutoa huduma na kituo pia kisajiliwe. Utoaji wa huduma bila usajili ni kukiuka sheria zilizowekwa.

“Wanatakiwa kufika katika ofisi za Baraza jijini Dodoma kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa usajili kabla ya huo muda tajwa,” amesema Ndahali.

Mwenyekiti msaidizi wa bodi ya baraza hilo, Dk Elizabeth Lema ametoa tafsiri ya tiba asili na tiba mbadala.

“Tiba asili ni zile ambazo tulirithi kwa mababu zetu na tiba mbadala ni zile ambazo watu wanasomea zinazotolewa kwa elimu rasmi,” amesema.

Baraza la tiba asili na tiba mbadala ndio baraza lenye mamlaka ya usajili na utoaji leseni kwa watoaji wa tiba hizo.