Wanataaluma ugavi, ununuzi waaswa kusimamia viapo
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo alipokuwa akihutubia katika mahafali ya 12 ya Wahitimu wa Mitihani ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi leo Jumamosi Oktoba 21, 2023 jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Wahitimu wa Mitihani ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi wameaswa kusimamia viapo vyao, kwani suala la maadili na weledi ni changamoto hususani katika sekta hiyo.
Dar es Salaam. Wahitimu wa Mitihani ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi, wameaswa kuzingatia maadili na weledi katika majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Jenifa Omolo katika mahafali ya 12 ya Wahitimu 269 wa Mitihani ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi yalifanyika leo Oktoba 21, jijini hapa.
Omolo amewata kusimamia viapo vyao, kwani suala la maadili na weledi ni changamoto hususani katika sekta hiyo ya ununuzi na ugavi kwa muda mrefu.
Amesema amefurahishwa kusikia kwamba taaluma hiyo inaendelea kuvutia wanafunzi wengi katika vyuo vya umma na binafsi nchini.
Pia amesema kumekuwa na uwiano mdogo kati ya wahitimu na wanafunzi wanaofanya mitihani kwa ajili ya kutambuliwa na bodi.
"Natoa wito kwa bodi kufanya hamasa kwa wahitimu wa vyuo kuongeza vichocheo kwa wahitimu ili kujiunga na mafunzo ya mitihani kitaaluma," amesema Omolo.
Aidha ameongeza kuwa ili kuendelea kuongeza ununuzi na ugavi bodi hiyo inapaswa kuongeza thamani ya programu zao ikiwa ni pamoja na kuongeza fursa za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri.
"Sisi kama wizara tutashirikiana nanyi katika kufanya mabadiliko chanya ya kuongeza thamani ya taaluma ili iweze kuwa na mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa," amesema Omolo.
Vilevile ameielekeza Bodi ya Wataalamu wa Mitihani ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kuchukua hatua zaidi ili kuimarisha usimamizi wa fani hiyo hususani katika kusimamia mitaala ya vyuo kwa lengo la kukuza weledi na maadili ya wahitimu.
Akizungumzia mtaala mpya uliozinduliwa katika mahafali hayo ambao unahusisha masomo mahususi ya maadili ya kitaaluma, Usimamizi wa mkataba, mali, ujuzi na ushauri elekezi kitaalamu na masuala ya kiongozi, Omolo amesema:
"Ninaipongeza bodi kwa kuandaa mtaala huu ambao utasaidia katika kutekelezeka mkakati wa Serikali wa kutekeleza ununuzi wa kimkakati," amesema Omolo.
Akizungumzia suala la ajira kwa wahitimu hao Omolo amesema tatizo la ajira ni changamoto ya nchi nyingi lakini Serikali Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inajitahidi kuweka mazingira mazuri kwa wataalamu mbalimbali wakiwemo wanunuzi hao ili kuweza kujiajiri.
"Niipongeze bodi kwa kuona umuhimu wa jambo hili na kuamua kuweka kozi za ujasiriamali kwenye mtaala wenu," amesema Omolo.
Pia amesema wahitimu hao wanapaswa kuitumia elimu waliyoipata ili kujiajiri na Serikali iko tayari kutoa ushirikiano utakaohitajika katika kufanikisha adhma hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Jacob Kibona amezitaja changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika kada hiyo.
Amesema kuna waajiri ambao wanaajiri wataalamu ambao hawajasajiliwa ambao hawatambuliki kisheria jambo ambalo linasabisha kushindwa kuwachukulia hatua za kinidhamu pale wanapokiuka taratibu za kimanunuzi.
"Kuna uwepo wa wadau mbalimbali wanaoingilia michakato ya ununuzi na ugavi hivyo kusababisha usumbufu Kwa Wataalamu walisajiliwa na kushindwa kufanya majukumu yao," amesema Kibona.
Kibona ameongoza kuwa kuporomoka kwa maadili katika jamii ni changamoto nyingine kwani wataalamu hao Wako Katikati ya jamii jambo ambalo ni rahisi kuathiri uadilifu wa wataalamu wa kada hiyo.
Naye mhitimu wa kozi ya Ununuzi na Ugavi kupitia mitihani ya kitaaluma ya PSPTB, Ester Mshana amesema licha ya changamoto ya ajira anaweza kutumia ujuzi alioupata kujiajiri.
"Kupitia elimu hii, tunafahamu ni vitu gani vya kufanya tunapoingia mtaani. Hata kama hakuna ajira Serikalini, masomo ya ujasiriamali tuliyosoma yanatupa uwezo wa kujiajiri," amesema Ester.