TPA yatoa zabuni ujenzi wa bandari mbili

Dar es Salaam. Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imetangaza zabuni mbili za ujenzi wa bandari ya Kisiwa Mgao mkoani Mtwara, Mbegani wilayani Bagamoyo, kadhalika bandari ya Tanga.

 Zabuni hizo, zinatangazwa kipindi ambacho kumekuwa na hoja kutoka kwa watu mbalimbali juu ya bandari zote nchini kukabidhiwa kwa kampuni ya Dubai ya DP World baada ya Tanzania na Dubai kuingia mkataba wa ushirikiano (IGA) wa kiuwekezaji katika bandari.

Katika tangazo la zabuni lililotolewa Septemba 8, mwaka huu TPA ilitangaza kusaka mkandarasi wa ujenzi wa bandari ya Mbegani huku ikieleza mwaliko wa mzabuni utatolewa Novemba mwaka huu.

 Tangazo lilitaka waombaji wote kutuma nyaraka za maombi kwa lugha ya kiingereza, baada ya kujisajili katika Mfumo wa Taifa wa Ugavi (Nest).

“Maombi yote yatumwe kupitia Nest kabla ya saa 2:00 PM Septemba 29, mwaka huu na yatafunguliwa mara tu yatakapotumwa na muombaji ataona ripoti ya mwenendo wa maombi yake,” ilieleza sehemu ya tangazo hilo lenye anuani ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.

 Tangazo jingine la zabuni ya ujenzi wa bandari Kisiwa Mgao, lilitolewa Septemba 14 na mwisho wa kutuma maombi ni Desemba 14 mwaka huu.

Ingawa Mwananchi halikuona tangazo la zabuni hiyo lakini Mbossa alisema kila jambo linakwenda kwa kufuata taratibu zinazotakiwa

“Watanzania wakae mkao wa kula kwa kuwa shughuli ndiyo imeanza na tayari tumeshatangaza zabuni nyingine katika bandari ya Tanga na nyingine zitakuja” alisema

“Serikali imekuwa ikisema bandari zote kutolewa si tafsiri sahihi ya mkataba, ule ni mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na Dubai katika kuendeleza bandari za Tanzania.

Alieleza mkataba wa IGA haumpi mwekezaji sehemu yoyote kisheria, bali unafungua milango ya majadiliano juu ya mikataba ya uwekezaji (HGA) na ile ya utekelezaji.

“Tunataka sasa ule mradi mkubwa wa kujenga bandari ya Bagamoyo ndiyo tumeanza hivi, tulishaweka katika bajeti lengo ni kuhakikisha ukuaji wa shughuli za kiuchumi unakutana na bandari ya kisasa kabisa yenye uwezo wa kupokea meli kubwa.”

Nyingine ambazo zabuni zake zitatangazwa, alisema ni Mbambabay, Kimondo, Bukoba, Mwanza, Tanga na Dar es Salaam watasaini mkataba wa kujenga kituo kikubwa cha kupokea mafuta.

Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Mtaalamu wa mikataba ya kimataifa, Dk Rugelemeza Nshalla alisema kinachoendelea katika pande mbili, inaweza kuwa ujanja kwa upande mmoja na pili unaweza kuwa uamuzi wa kisheria wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Nshalla alidai kuwa sehemu ya pili ya mkataba huo (IGA) imeweka wazi kwamba unahusisha bandari zote za Tanzania sasa iweje itangazwe zabuni kwa wengine.

“Ni ujanja ujanja tu kwa sababu IGA imejieleza wazi, lakini hata agizo la Rais Samia ndani ya mkataba unaeleza bandari zote,” alisema Dk Nshalla.

kwa upande wake, mtaalamu wa Sheria, Profesa Issa Shivji pamoja na kukiri kuwa sehemu ya pili ya mkataba wa IGA umetoa bandari zote nchini, lakini alisema ni vigumu kulielezea hilo kwa kuwa mikataba mingine iliyopo haijulikani inasema nini.