Wanawake wametakiwa kushirikiana kufikia fursa za uongozi

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini Mkoa wa Pwani Mwajuma Nyamka (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Taasisi ya Mfuko wa Mama Samia. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

Umeelezwa kuwa, wanawake wameanza kubadilika kwa  kuongeza upendo ni vema mwelekeo huo ukaendelea hivyo

Kibaha. Wanawake wametakiwa kudumisha mshikamano, upendo na ushirikiano miongoni mwao ili kuzifikia nafasi za uongozi wa siasa nchini.

Hayo yamebainishwa leo Machi 9, 2024 na Mwenyekiti wa  Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini Mkoa wa Pwani, Mwajuma Nyamka wakati wa uzinduzi wa Mfuko wa Mama Samia wa Kishindo cha Mama.

"Zamani tulikuwa tunasema adui wa mwanake ni mwanamke, lakini kila tunavyoendelea tunaona kuna mwelekeo wa mabadiliko, wanawake wameanza kubadilika kwa kuongeza upendo ni vema mwelekeo huo ukaendelea hivyo," amesema Nyamka.

Amesema iwapo kundi hilo litaendelea kuweka kando mambo ya mgawanyiko na fitina miongoni mwao kutawawezesha Serikali kuendelea kuwafikiria na kuongeza fursa nyingi zitakazowapa nafasi ya kujiendeleza kiuchumi

"Kuna fursa ambayo Serikali imeleta kwa kipindi kirefu, lakini huenda wengi hawaijui ya jukwaa la uwezeshaji kiuchumi wanawake, huko kuna faida nyingi ikiwamo kupata mitaji ya biashara na hata ubunifu, hivyo nawahimiza jiungeni huko ili mpate kueleweshwa na kufaidi fursa zilizoko humo,” amesema Nyamka.

Awali,mwenyekiti wa taasisi hiyo, Asha Baraka amesema lengo la kuanzishwa taasisi hiyo inayohusisha wanawake pekee ni kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na hata masuala ya siasa.

"Tuna malengo mbalimbali ikiwamo kusaidiana katika nyanja za kijamii kiuchumi na kushiriki shughuli za Serikali, hata vyama vya siasa na ndio maana humu tumechanganyika watu wa taaluma na fani mbalimbali, hivyo kila mmoja atakuwa na umuhimu wa kutoa mchango wake wa mawazo na ujuzi wake ili tufikie malengo," amesema Asha.

Pia, amesema mpaka sasa wana jumla ya wanachama 50 na tayari wameshapata usajili rasmi serikalini na bado wanaendelea kukaribisha wenye nia ya kujiunga ili kuwa na kundi kubwa kwa kuwa rasilimali watu ni kitu muhimu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mailimoja B, Shauri Yombayomba amesema Serikali inatoa fursa nyingi kwa vikundi vilivyosajiliwa, hivyo ni vyema wanachama hao wakaishi kwa kufuata malengo waliyojiwekea ili kuendelea kuaminika.

Ingawa Serikali imekuwa ikiweka mipango na taratibu mbalimbali zinazowawezesha wanawake kupata uongozi katika nyanja za siasa ikiwamo nafasi za viti maalumu ndani ya Bunge, pia sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000 iliongeza chachu kwa kundi hilo kuendelea kuthaminika.