Wanne kati ya 88 waripoti kuanza kidato cha kwanza

Wanafunzi wanne kati ya 88 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Izumachel iliyopo wilayani Geita

Muktasari:

Ikiwa wiki moja imepita tangu kuanza kwa msimu wa masomo mwaka 2023 Tanzania, wanafunzi wanne kati ya wanafunzi 88 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Izumachel iliyopo wilayani Geita mkoani hapo ndio walioripoti katika shule hiyo.


Geita. Ikiwa wiki moja imepita tangu kuanza kwa msimu wa masomo mwaka 2023 Tanzania, wanafunzi wanne kati ya wanafunzi 88 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Izumachel iliyopo wilayani Geita mkoani hapo ndio walioripoti katika shule hiyo.

Shule hiyo iliyoanza mwaka 2022 ikiwa na wanafunzi 40 wa kidato cha pili hadi sasa walioripoti na kuanza masomo ni wanafunzi 26 na kufanya shule nzima kuwa na wanafunzi 30 kati ya 128 walioachaguliwa kujiunga na shule hiyo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea shule hiyo Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Thomas Dime amewataka viongozi wa vijiji kupita nyumba kwa nyumba kuwasaka wanafunzi hao ili waanze masomo.

 “Kuna watendaji wa vijiji na kata yupo afisa elimu kata sijui mnafanya nini shule zimefunguliwa hakuna wanafunzi na nyie mpo tuu hakuna hatua mnazochukua nataka muwasake wazazi hata kama mwanafunzi hana sare ya shule avae zile za msingi aingie darasani wakati ambao mzazi anapambana kupata sare za sekondari” amesema Dime.

Naye, mkuu wa shule ya sekondari Izumachel, Edward Nkwabi amesema changamoto kubwa katika eneo hilo ni mwamko mdogo wa elimu kwa wazazi pamoja na shule kuchukua watoto wanaotoka katika visiwa vitatu tofauti hivyo kulazimika kupanga mtaani.

Wakizungumza baadhi ya wanafunzi akiwemo, Simon Malula amesema kutohudhuria kwa wanafunzi hao kumesababisha wasifundishwe wakilazimika kuwasubiri wenzao waripoti.

“Nikikutana na wenzangu waliochaguliwa kusoma hapa wanasema hawana vifaa vya shule ndio wanasubiri wanunuliwe ili waje lakini kuna wengine wanasema wao hawataki kusoma wapo tuu mtaani” amesema Malula.