Wanne kati ya watano kidato cha pili Temeke wapata daraja la nne na sifuri

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk Said Mohammed

Muktasari:

  •  Asilimia 80.75 ya wanafunzi waliofanya mtihani kidato cha pili mwaka jana wilayani Temeke walipata daraja la nne na sifuri huku walimu kukosa motisha katika ufundishaji, kukosekana kwa miundombinu toshelezi ya kujifunzia, kukosekana kwa hamasa ya elimu kwa wazazi wa eneo hilo vikitajwa kuwa sababu.

Dar es Salaam. Angalau wanafunzi wanne kati ya watano waliofanya mtihani wa kidato cha pili katika wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam mwaka 2023 walipata daraja la nne au sifuri, jambo ambalo wadau wanasema lisipofanyiwa kazi watakaofeli kidato cha nne watakuwa wengi.

Matokeo hayo yana maana mwanafunzi mmoja kati ya watano alipata daraja la kwanza hadi la tatu.

Anguko hilo, linatajwa kuchangiwa na walimu kukosa motisha katika ufundishaji, kukosekana kwa miundombinu toshelezi ya kujifunzia, kukosekana kwa hamasa ya elimu kwa wazazi wa eneo hilo jambo linalokwenda sambamba na ukumbatiaji wa mila na desturi.

Wadau wa elimu wameeleza kama jitihada za makusudi hazitafanyika, matokeo hayo ndiyo yanaakisi kile kitakachopatikana katika mtihani wa Taifa kidato cha nne kwa sababu wote waliopata daraja la nne wataendelea kidato cha tatu.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, wanafunzi 16,793 ndiyo walioketi katika mtihani huo ulioanza Oktoba 30 hadi Novemba 9, 2023.

Kati ya wanafunzi hao 3,231 ndiyo walipata daraja la kwanza hadi la tatu ikiwa ni sawa na asilimia 19.24.

Waliobakia ambao ni daraja la nne na sifuri walikuwa asilimia 80.75 lakini katika mchanganuo, asilimia 66 ambao ni sawa na wanafunzi 11,121 walipata daraja la nne.

“Tuwe kama wazazi, sijafurahishwa na matokeo haya, kiuhalisia na mtazamo wa kawaida tunaonekana tumefaulu kwa asilimia ya 80.75 lakini katika uchambuzi tumefeli,” amesema Mapunda alipokutana na wasimamizi wa elimu wilayani humo.

Katika mkutano huo uliojumuisha wakuu wa idara, wathibiti wa ubora wa elimu na walimu wa shule za sekondari Manispaa ya Temeke, Mapunda alitoa siku saba ili wajitathmini ili baada ya miaka miwili waweze kupindua meza.

“Kwa hali iliyopo, hakuna matumaini ya watu hao kupata daraja la kwanza na badala yake wataangukia daraja sifuri kama hakutakuwa na mkakati wa makusudi.

Baada ya tathmini hiyo na kikao atakachokifanya na wakuu wa shule za msingi mwishoni wiki hii, kama wilaya inatarajia kuja na mkakati wa pamoja wa kuboresha ufaulu.

Akizungumzia suala hilo, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten/Met), Ochola Wayoga amesema kile kilichopatikana katika matokeo haya kinaakisi kile kitakachopatikana kidato cha nne baada ya miaka miwili.

Hiyo ikiwa na maana, asilimia 66 ya wanafunzi waliopata daraja la nne wanahesabika wamefaulu kuendelea kidato cha tatu na wale 2,441 waliopata daraja sifuri ndiyo watakaorudia darasa.

Katika hilo, Wayoga amesema mzigo mkubwa wa walimu katika ufundaji unaweka ugumu wa kumfikia mwanafunzi mmoja mmoja huku akitaka miundombinu ya kujifunzia iimarishwe.

“Serikali iwekeze katika vitabu, madarasa ya kutosha sehemu nyingine wanafunzi bado wanasubiriana nje wengine watoke darasani ili wao waingie kufanya mtihani.

Kwa upande wake, Neema Kitundu ambaye ni mdau wa elimu amesema mila na desturi zinazopatikana katika wilaya hiyo, kukosa mwamko wa elimu kwa wazazi, shida ya usafiri kwa wanafunzi, maadili kwa watoto kuwa chini ndiyo sababu za kuwapo kwa matokeo hayo duni.

“Walimu wenyewe wanakata tamaa kutokana na mmomonyoko wa maadili kwa watoto, zamani ilikuwa mtoto wa mwenzio ni wako lakini sasa ukijaribu kumuonya mzazi wake atakujia juu,” amesema Neema.

Neema ambaye pia anatokea asasi ya  Forum for African Women Educationalists (FAWE) Tanzania, amesema kukosekana kwa mbinu za ufundishaji kwa walimu hao ni sababu nyingine ya ufaulu duni.

“Wengi wanakosa mbinu bora za ufundishaji, walizonazo ni wachache sana ambao wanaweza kukidhi mahitaji ya wanafunzi,’ amesema Neema.

Nini Kifanyike

Wayoga amesema ili kuondokana na suala hilo, walimu wapewe vigezo vya utendaji vipya kwenye ufundishaji, wapimwe uelewa wao juu ya kile wanachokifundisha, na kupewa motisha katika ufundishaji ili waweze kujitoa zaidi.

“Walimu waone aibu, shule yako inatoa daraja la nne wengi na sifuri kuliko daraja la kwanza hadi la tatu.

Alitaka pia wanafunzi wahamasishwe juu ya umuhimu wa elimu.

Suala hilo liliungwa mkono na Neema ambaye alieleza umefika wakati sasa wazazi wakajengewa uelewa juu ya malezi, maadili na kujitambua ili waweze kufuatilia maendeleo ya wanafunzi.

“Walimu pia wajengewe uwezo, wapewe motisha ili waweze kujituma zaidi kwa sababu baadhi ya mazingira yanawakatisha tamaa hasa ukizingatia wengi waliosoma ualimu kwa miaka ya karibuni walienda ili wapate urahisi wa mikopo siyo kwa wito kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” amesema Neema.

Pia aligusia suala la kuwajengea uwezo wanafunzi juu ya kujitambua wao ni kina nani, wanafanya nini na wanataka kwenda wapi ili waweze kuepukana na tamaa ya kupata kipato cha haraka.

Matokeo kwa baadhi ya shule

Baadhi ya shule ambazo wanafunzi wake walifanya mtihani huo ipo ile ya Sekondari Diplomasia ambayo haikuwa na daraja la kwanza wala la pili huku mwanafunzi mmoja pekee ndiyo aliyepata daraja la tatu, 365 wakiwa na daraja la nne na 212 wakiangukia daraja sifuri.

Shule ya sekondari Uhamiaji wanafunzi watano walikuwa na daraja la kwanza, 9 walikuwa na daraja la pili, 36 daraja la tatu, 423 walikuwa na daraja la nne huku 59 wakiwa na daraja sifuri.

Mikwambe, mwanafunzi mmoja alikuwa na daraja la kwanza, 16 daraja la pili, 27 daraja la tatu, 358 daraja la nne na 273 wakiwa na daraja sifuri

Mbande, wanafunzi 24 walikuwa na daraja la kwanza, 42 daraja la pili, 50 daraja la tatu, 514 daraja la nne na 76 daraja sifuri.Shule ya sekondari Kurasini wanafunzi mmoja ndiyo alikuwa na daraja la pili, wawili daraja la tatu, 499 daraja la nne na sifuri wakiwa wanafunzi 114.

Taifa sekondari wanafunzi 9 walipata daraja la kwanza, 29 wakipata daraja la pili, 39 daraja la tatu, 493 wakipata daraka la nne na 29 wakiwa na daraja sifuri.