Wanne wa familia moja wafa kwa kula kasa Zanzibar

What you need to know:

  • Ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu watu saba kufariki dunia na wengine 24 kulazwa kisiwani Pemba kwa kula samaki aina ya kasa, jana Jumamosi Desemba 25, 2021 watu wanne wa familia moja wamefariki dunia na wengine 47 kulazwa baada ya kula samaki huyo.

Unguja. Ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu watu saba kufariki dunia na wengine 24 kulazwa kisiwani Pemba kwa kula samaki aina ya kasa, jana Jumamosi Desemba 25, 2021 watu wanne wa familia moja wamefariki dunia na wengine 47 kulazwa baada ya kula samaki huyo.

Tukio la Pemba lilitokea wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba Novemba 25, 2021 na hili na leo limetokea Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Martin Otieno amesema leo kuwa tukio hilo limetokea Desemba 22 maeneo ya Matamwe baada ya kasa huyo kuvuliwa akiwa kando ya Bahari ya Hindi..
Waliofariki wote ni watoto wa familia moja huku waliolazwa nao wengi wao ni watoto chini ya umri wa miaka 18.

"Kuna mvuvi anaitwa Juma Mussa (30), alimuona kasa alikuwa anataga mayai katika maeneo hayo, alimtoa akisaidiana na wananchi wengine wakamchinja na kugawana kitoweo chake," amesema.
Hata hivyo kamanda Otieno amesema madhara yalianza kuonekana baada ya mtoto wa mvuvi huyo Mohamed Juma kufariki dunia ndipo mashaka yalianza kuwaingia zaidi na kuanza kujisikia vibaya wakakimbizwa hospitalini.

Kwa mujibu wa kamanda Otieno, wakiwa hospitali ya Matemwe watoto wengine watatu, Ali Juma (4), Juma Musa (6) na Zainabu Juma mwenye umeri wa mwaka mmoja walifariki dunia.

Amesema mpaka sasa wapo watu 47 wanaoendelea na matibabu katika hospitali  ya Kivunge kati ya hao watoto wenye umri chini ya miaka 18 ni 31 na wengine 16 ni watu wazima.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.