Wanne wakiwemo askari polisi wafariki kwa ajali Njombe
Muktasari:
- Wanne hao wamefariki dunia kwenye ajali mbili tofauti moja ikihusisha askari polisi wawili eneo la Isoliwaya wilayani Wanging'ombe na nyingine ikihusisha lori la mizigo.
Njombe. Watu wanne wamefariki dunia wakiwemo askari polisi wawili wa usalama barabarani, kutokana na ajali mbili tofauti zilizotokea leo hapa mkoani hapa.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Desemba 4,2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema ajali ya kwanza imetokea saa 12:20 asubuhi katika Kijiji cha Isoliwaya kilichopo kata ya Wanging'ombe Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe Barabara Kuu ya kuelekea mkoani Mbeya, ambapo ajali hiyo ilihusisha magari mawili moja gari ndogo aina ya Toyota Sienta na gari nyingine aina ya Sharpman iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zambia.
Amesema chanzo cha ajali hiyo ni gari ndogo iliyokuwa ikiendeshwa na askari polisi kutochukua tahadhari wakati ikiipita gari nyingine na kwenda upande wa pili, jambo ambalo lilisababisha magari hayo kugongana.
"Gari ndogo wakati inatoka pembeni iligongwa upande wake wa kushoto na ndani ya hiyo gari kulikuwa na abiria ambaye naye alikuwa askari polisi na walikuwa wanaenda kutekeleza majukumu yao ya kawaida," amesema Banga.
Amesema waliofariki kwenye ajali ni Elizabia Kizale (35) mwenyeji wa Chunya mkoani Mbeya na Patrick Salehe (34) mwenyeji wa Lushoto huko mkoani Tanga.
Amesema dereva wa Sharpman ametoroka na jeshi hilo linaendelea na jitihada za kumtafuta kwa ajili ya taratibu zingine za mahojiano.
Amesema ajali nyingine imetokea saa 3:30 asubuhi eneo la Igawilo, Kata ya Kifanya Halmashauri ya Mji wa Njombe ambapo lori aina ya Howo lenye tela, liligongana na gari ndogo Toyota VXR na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi wawili.
"Watu wawili waliokuwa kwenye gari ndogo wakiwa wanapatiwa matibabu kwenye hospitali ya mkoa inayofahamika kama Wikichi wamefariki," amesema Banga.
Amesema waliofariki kwenye ajali hiyo ni Luno Nyika (43) mkazi wa Mbinga na Scholastica Nyika (35) ambaye ni mwenyekiti wa kijiji huko Mbinga.
Amesema majeruhi ambao wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya Kibena ni Oscar Mgovani (43) dereva wa gari ndogo na Faraja Nyika (17) mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana pamoja na utingo wa gari kubwa Tarick Mohamed (20), na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.
Amesema dereva wa lori hilo naye alikimbia baada ya ajali hiyo kutokea na jeshi linaendelea kumtafuta kwa ajili ya taratibu zingine za uchunguzi.
Amesema jeshi hilo linatoa wito kwa magari yote kuchukua tahadhari wakati wanatumia barabara kwa kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani pamoja na alama zake.
Amesema maeneo mengi ya mkoa huo yana miteremko mikali na miinuko, hivyo madereva wanatakiwa kuwa makini ili kuepusha ajali ambazo zinaweza kuzuilika.