Wapewa mbinu kilimo cha Maharage

Rukwa/Songwe. Wakulima wa zao laMaharage katika mikoa ya Rukwa na Songwe wamehimizwa kujikita kwenye kilimo himilivu kinachoendana na hali ya hewa sambamba na kujitoa ili kupata mavuno ya uhakika.
Kwa kutambua hilo Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali za Sweden na Denmark kupitia, Taasisi ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo nchini (AMDT) na Kampuni ya pembejeo ya Ikuo General Enterprises ya mikoa hiyo kwa pamoja wamehimiza wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na kuhamia kwenye kilimo cha kisasa ambacho wao ndio wasimamizi.
Kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia na Tanzania ikiwemo, kumekuwa na changamoto kwa wakulima wanaotegemea mvua za misimu, wasiotumia mbolea sahihi hivyo kuleta ugumu katika mnyororo mzima kwanzia kupanda hadi kuvuna.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mwishoni mwa wiki shamba la moja ya mkulima aliyehamia kwenye kilimo cha kisasa cha zao la Maharage, ofisa Kilimo kutoka kampuni ya Ikuo, Innocent Bungwa alisema ni wakati sasa wakulima kubadili fikra, ingawa wengi wameanza kuhamia kwa wingi.
Alisema hadi sasa kuna wakulima zaidi ya 8000 ambao wameshapata elimu ya kilimo cha kisasa na himilivu kinachoendana na mabadiliko ya tabianchi lakini bado wanapaswa wakulima wote wajikite huko.
"Mkulima kwanza anapaswa ajitoe, abadili fikra apate ushauri, kama tunavyofanya ili abadilike", alisema Bungwa.
Alisema wanawahimiza wakulima kutumia mbegu bora za maharage kama, Mwaspenjere, Njano Uyole ambazo zinavumilia hali ya hewa.
Bungwa alisema muitikio wa wakulima ni mkubwa na wao kama kampuni ya pembejeo inayofanya kazi na Taasisi ya AMDT wanatoa huduma ya ushauri wa hali ya hewa na huduma ya utambuzi wa afya ya udongo kwa wakulima.
Akizungumza alipokuwa shambani, kata ya Ndalambo mkoani Songwe, Furaha Kibona ambaye ni mkulima wa mfano wa zao la Maharage aliyekubali kuhamia kwenye kilimo himilivu alisema alijifunza elimu ya kilimo hicho kupitia mradi wa AMDT na akaamua kujitoa.
Kibona alisema baada ya kutumia kilimo himilivu sasa anatarajia kupata gunia zaidi ya 10 baada ya kuwa anapata gunia 3, hadi 4 kwa ekari moja hapo zamani.
Kibona anasema hawezi kurudi tena kwenye kilimo cha mazoea na anawahimiza wakulima wenzie kubadilika, aidha ameiomba Serikali kupunguza gharama za pembejeo.
Ofisa Kilimo mwingine kutoka Ikuo mkoani Rukwa wilaya ya Sumbawanga, Amos Songoro alisema kutokana na wakulima kupanda mbegu zisizo bora imewapelekea kukosa soko kutokana na kupata mavuno madogo na yasiyo bora, ndio maana wameamua kutoa mafunzo, huduma na ushauri ili wabadilike.
Songoro alisema kupitia mradi wameshawafkia wakulima zaidi ya 12,000 katika mikoa hiyo kupitia mafunzo mbalimbali ikiwemo ya Shamba darasa na progamu za redio.
Naye mkulima mwingine wa maharage kutoka Sumbawanga, Osward Mtindya alisema kwa sasa anapokea wakulima wapya watatu kila siku ambao wanahitaji elimu ya kilimo himilivu ingawa angependa wakulima wengine wazidi kujutokeza