Wasaka tiba migogoro ya wanyamapori, binadamu
Muktasari:
- Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2012 hadi 2019, watu 642 wamejeruhiwa huku watu 1,069 wamepoteza maisha na mifugo 792 ikiuawa, pamoja na ekari 41,401 za mazao kuharibiwa, kutokana na migogoro hiyo ya binadamu na wanyama.
Arusha. Zaidi ya wataalamu 300 wa masuala ya uhifadhi na wanyamapori kutoka mataifa 22 duniani, wanatarajia kukutana jijini Arusha, kusaka suluhu ya migogoro baina ya wanyama na binadamu.
Wataalamu hao wanatarajia kukutana katika mkutano wa 14, wa kisayansi ulioandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (Tawiri), na unatarajia kufanyika kwa siku tatu kuanzia Desemba 6, 2023; jijini Arusha.
Akizungumzia mkutano huo leo Desemba 2, 2023, Mkurugenzi wa Tawiri, Dk Ernest Mjingo amesema mkutano huo unatarajia kuangazia namna bora ya utatuzi wa migogoro baina ya wanyamapori na binadamu kwa kubadilishana uzoefu.
Amesema migogoro hiyo inayotokea baina ya wananchi wanaoishi ndani au karibu na hifadhi za wanyama hao na kwamba imekuwa tishio kutokana na madhara mbali mbali yanayojitokeza ikiwemo uharibifu wa mali na mifugo, pia vifo vya binadam na wanyamapori.
"Tutajadili hasa migongano ya wanyamapori na binadamu na namna ya kutatua changamoto hiyo ambayo chanzo chake ni shughuli za binadamu kuingilia na kuharibu bionuwai na kuziba shoroba za wanyamapori lakini pia mabadiliko ya tabianchi," amesema.
Kwa mujibu wa bosi huyo wa Tawiri, dunia inapambana na kurudisha mazingira ya asili yaliyoathiriwa na binadamu ambapo inadaiwa zaidi ya spishi 41,000 za wanyamapori kupotea, huku wengine wakiwa katika hatari ya kutoweka.
Amesema kauli mbiu ya mkutano huo ni: “Maisha jumuishi kati ya binadamu na wanyamapori kwa ajili ya maendeleo ya uhifadhi na bionuwai kwa ujumla, kwa maendeleo ya jamii tuliyonayo’’.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Tawiri, Dk Julius Keyyu, amesema migogoro kati ya wanyamapori na binadamu ni muingiliano kati ya pande hizo mbili, ambayo huweza kuleta uhusiano hasi kati yao.
"Wanyama ambao huleta mgongano na migogoro hii kwa asilimia kubwa ni kama simba, tembo, fisi, chui na wengine wadogo kama nyani, ngedere na ndege," amesema Dk Keyyu.
Keyyu anaamini kuwa migogoro mingi husababishwa na mambo kadhaa ikiwemo ongezeko la makazi na idadi kubwa ya watu, na hivyo kusababisha shughuli za kilimo kufanyika kwenye shoroba au mapito ya wanyama.
Visababishi vingine vya migogoro kwa mujibu wa mkurugenzi huyo wa utafiti katika taasisi hiyo, ni uingizaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi, mabadiliko ya hali ya hewa yanayoleta ukame na njaa kwa wanyama na hivyo kuamua kuvamia maboma kusaka mahitaji yao.
Aidha takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2012 hadi 2019, watu 642 wamejeruhiwa nchini huku watu 1,069 wamepoteza maisha na mifugo 792 ikiuawa, pamoja na ekari 41,401 za mazao kuharibiwa, kutokana na migogoro hiyo ya binadamu na wanyama.