Wasakwa kwa kuiba Sh31. 2 milioni kisha kujeruhi walinzi
Muktasari:
Jeshi la Polisi mkoani Geita linawasaka watu wasiojulikana waliovamia na kupora maduka yanayotoa huduma za kifedha katika eneo la soko kata ya Nyawilimwilwa wilaya ya Geita kisha kupora Sh31.2 milioni na kujeruhi walinzi saba waliokuwa wakilinda maduka hayo.
Geita. Kundi la watu 10 wanaosadikika kuwa wezi wamevamia na kupora maduka nane ya huduma za kifedha yaliyopo kata ya Nyawilimwilwa Wilaya ya Geita na kuiba Sh 31.2 milioni kisha kuwajeruhi walinzi saba waliokuwa wakilinda maduka hayo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Berthaneema Mlay amesema tukio hilo limetokea April 23, 2023 Saa 9 alfajiri ambapo kundi hilo linalodaiwa kuwa la vijana lilivamia eneo la soko na kufanya uhalifu huo.
Amesema kabla ya kuvunja maduka hayo ya huduma za fedha waliwashambulia walinzi kwa kutumia silaha za jadi yakiwemo mapanga ambapo mlinzi mmoja alijeruhiwa kichwani na kitu chenye ncha kali.
“Nitoe wito kwa wananchi kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili washirikiane na polisi kuimarisha ulinzi lakini wamiliki wa maduka wekeni walinzi wenye viwango kulinda biashara zenu hawa walinzi kama wangekuwa na silaha wangeweza kuwadhibiti wahalifu hawa”amesema Mlay
Katika tukio jingine watu watano wakazi wa kata ya Kakola wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuchoma nyuma mbili za Juma Masanja wakimtuhumu kuwa ni mwizi sugu.
Kamanda Mlay amedai watu hao wanadaiwa kuchoma nyumba hizo baada ya kugundua mmiliki hayumo ndani na kuwa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini walioiba kwenye maduka ya huduma za kifedha sanjari na kuwakamata waliochoma nyumba ya Musa ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.