Wasichana 20,759 chini ya miaka 14 kupatiwa chanjo HPV

Muktasari:

  • Shirika la Afya Duniani (WHO) liliidhinisha chanjo hiyo itumike Tanzania tangu mwaka 2014

Missenyi. Wasichana 20,759 katika Halmashauri ya Wilaya Missenyi mkoani Kagera, wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya HPV kuwakinga dhidi ya saratani ya shingo kizazi.


Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 16, 2024 na mratibu wa huduma za chanjo wa Halmashauri ya Wilaya Missenyi, Edward Kagari kwenye kikao cha kujadili namna chanjo hiyo itakavyotolewa.

Amesema chanjo hiyo itaanza kutolewa Aprili 22 hadi 28, 2024  na walengwa ni watoto wa kike wenye umri wa  kuanzia miaka tisa mpaka 14.

“Kazi hii tutaifanya kwa siku tano, wataalamu wetu watapita maeneo mbalimbali ambayo ni pamoja na shuleni, nyumbani , sokoni na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu watatoa elimu sambamba na kutoa chanjo hiyo,” amesema Kagari.

Hata hivyo, Kagari amesema kwa kipindi cha miaka mitano hawajawahi kupokea msichana yeyote kwenye vituo vya afya na zahanati zote mwenye  tatizo la saratani ya shingo ya kizazi.

Ofisa Mpango wa Chanjo na Mratibu wa Shughuli za Shirika  la JHPIEGO Tanzania,  Emmanuel Tesua amesema kupitia mradi wa MCGL unaofadhiliwa na USAID   watahakikisha wanatoa hamasa ya kufanikisha kazi hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali mstaafu Hamis Maiga amehimiza viongozi wote wakiwamo watendaji wa kata, vijiji, viongozi na wale wa dini sambamba na wataalamu wa afya, kutoa hamasa ya upatikanaji wa walengwa kwenye maeneo yao ili waweze kupatiwa chanjo hiyo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) liliidhinisha chanjo hiyo itumike Tanzania tangu mwaka 2014 na Tanzania ilianza kutumia chanjo hiyo Mkoa wa Kilimanjaro kwa wasichana waliokuwa na umri chini ya miaka 14 kupatiwa  kuwapatia dozi mbili.