Wasichana 271,650 kupatiwa chanjo ya HPV Kagera

Baadhi ya wataalamu wa afya Mkoa wa Kagera,  wakipewa  maelekezo kwenye kikao cha uelewa kuhusu jinsi ya hatua ya utoaji chanjo hiyo itakavyofanyika mkoani humo.

Muktasari:

  • Chanjo hiyo itaanza kutolewa rasmi Aprili 22, 2024 hadi Aprili 28, 2024 na walengwa ni watoto wa kike wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi 14.

Kagera. Wasichana 271,650 watapatiwa   chanjo ya HPV mkoani hapa kwa lengo la kuwakinga na saratani ya shingo kizazi.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi  Aprili 18, 2024 na mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dk Baraka Egnatus katika shughuli ya kutoa elimu kuhusu chanjo ya HPV itakayotolewa kwa wasichana hao walio chini ya umri wa miaka 14.

Amesema chanjo hiyo itaanza kutolewa rasmi Aprili 22, 2024 hadi Aprili 28, 2024 na walengwa ni watoto wa kike wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi 14.

“Nipo hapa kwa ajili ya kampeni ya  kuhakikisha wasichana wote hapa nchini walio  chini ya miaka 14 wanakingwa dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa kuwapatia chanjo hii ya HPV na tumeona ili kufikia angalau asilimia 85 ya wasichana ambao wapo kwenye umri huo, tutumie wiki moja kuwatambua,” amesema Dk Baraka.

Mganga Mkuu wa Mkoa Kagera, Dk Samwel Raizar amesema kupitia idara ya afya umejipanga kwa kuanza kuwapatia mafunzo wote watakaohusika katika kutoa chanjo hiyo.

Katibu Tawala wa Mkoa Kagera, Stephen Mashauri amesema chanjo hiyo itakayoanza kutolewa katika kilele cha chanjo itumike kuhakikisha wananchi wanahamasika kuwakinga watoto walio  chini ya umri wa miaka 14 waliolengwa kufikiwa.