Wataalamu: Kuchoma chanjo ya Uviko-19 zaidi ya moja hakuna madhara

Wataalamu: Kuchoma chanjo ya Uviko-19 zaidi ya moja hakuna madhara

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya wamesema mtu kupata chanjo tofauti za kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 hakuwezi kumletea madhara na badala yake huongeza ufanisi wa kinga za mwili dhidi ya virusi vya ugonjwa huo.


Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamesema mtu kupata chanjo tofauti za kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 hakuwezi kumletea madhara na badala yake huongeza ufanisi wa kinga za mwili dhidi ya virusi vya ugonjwa huo.

Wametoa ufafanuzi huo siku chache baada ya nchi ya Saudi Arabia kuwataka mahujaji wanaotaka kwenda Hijja waliochoma chanjo ya Sinovac, kuchoma chanjo nyingine ambazo nchi hiyo ilizitaja kuwa ni Astrazeneca, Pfizer na Johnson & Johnson.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Septemba Mosi, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shadrack Mwaibambe amesema chanjo aina moja haitakiwi kuchomwa zaidi ya mara moja, lakini mtu anaweza kuchoma chanjo za aina nyingine.

Amesema tafiti zinaonyesha mtu akichanja chanjo aina mbalimbali zinaongeza ufanisi kwa kuwa zimetengenezwa tofauti na zina ubora tofauti.

“Ni vizuri, hakuna madhara yoyote na inafanya kazi zaidi, chanjo tofauti huleta matokeo mazuri,” alisema.

Akizungumzia changamoto kwa nchi mbalimbali kutaka watu wachanje chanjo wanazozitaka wao, alisema hiyo inatokana na unyanyapaa kwamba kuna baadhi ya nchi zinaona chanjo ya aina fulani ndiyo bora.

“Ukiangalia chanjo ya Sinovac, Saudi Arabia wameikataa lakini pia ubora wake upo chini, lakini pia ni nchi husika kujikuza kwamba ipo kiwango cha juu. Hata Uingereza ina chanjo yake ambayo baadaye wamekataa mataifa mengine yasizalishe, ukiangalia kwa undani hizi chanjo zinakuja kama biashara na kila mtu anajaribu kuliteka soko.

“Uingereza walitoa kibali India izalishe, lakini sasa ukichoma ya India hawatakuruhusu uingie nchini kwao,” alisema.

Dk Mwaibambe alisema suala la chanjo lina mkanganyiko mkubwa na kwamba Watanzania itawachukua muda kulielewa, hivyo ni vema sasa kila mmoja achanje hasa wale wanaosafiri kwenda mataifa mbalimbali.

Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati alisema kuna uwezekano kwa mtu aliyechanja chanjo aina moja inayokinga Uviko-19 kutaka kuongeza chanjo ya pili.

Amesema tafiti bado zinaendelea kuhusu ufanisi zaidi iwapo mtu atachanjwa kwa mara nyingine na iwapo atachanganya chanjo tofauti.

“Nawajua watu wamechomwa chanjo aina mbili tofauti lakini wanaendelea vizuri tu kikubwa tusubiri majibu yake yatatoka hivi karibuni,” amesema Dk Osati.

Kuhusu mambo yanayojitokeza ya aina tofauti za chanjo na ruhusa zake katika baadhi ya nchi,amesema hizo ni siasa, kwani kila nchi inajaribu kupigia upatu chanjo yake.

“Ukisema Sinovac haitambuliki WHO (Shirika la Afya Duniani) inaitambua ndiyo maana imewekwa kwenye orodha ya chanjo ambazo zinaweza kutolewa. Ni siasa tu za kimatibabu zinazoingilia utaalamu,” amesema.

Baadhi ya Watanzania wanaotaka kwenda kuhiji hasa waliopo visiwani Zanzibar, sasa wanalazimika kuchoma chanjo kwa mara nyingine, ili kuendana na masharti yaliyowekwa Saudi Arabia.

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema wanaotaka kwenda Hijja ambao wamechoma chanjo hiyo awali watalazimika kuchoma tena chanjo ya Johnson & Johnson kwa sababu Saudia haiitambui chanjo ya Sinovac.

Chanjo ya Sinovac ikiwa ni miongoni mwa zile zilizopitishwa na WHO ilianza kutolewa Zanzibar Julai 23 mwaka huu.