Watafiti wagundua viuatilifu vya kuangamiza mmea hatari nchini

Mmea wa gugu karoti kitaalamu ni Parthenium hysterophorus ambao umepatikana viwatilifu vya kuuangamiza baada ya utafiti wa zaidi ya miaka 13.

Muktasari:

  • Mmea hwa gugu karoti umeonekana nchini mwaka 2010 ambapo baada ya utafiti umebainika kuwa na madhara makubwa kwa kudidimiza mazao, kuua baadhi ya mifugo lakini kusababisha magonjwa ya mzio, macho na Kansa kwa binadamu, hatimaye umepatiwa ‘mwarobaini’ 

Arusha. Wanasayansi kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) wamefanikiwa kubaini viuatilifu vinavyoweza kuangamiza mmea hatari nchini ujulikanao kama 'gugu karoti'.

Akizungumza na Mwananchi, kaimu Mkurugenzi wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema kuwa utafiti wa kuangamiza mmea huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 13 sasa ulipitia ngazi tofauti hadi kufikia mafanikio hayo.

Amesema mmea huo unaojulikana kwa jina la Gugu karoti kitaalamu unajulikana kama ‘Parthenium hysterophorus’ unaweza kuangamizwa na viuatilifu aina ya 2,4-D-Triclopyr na Gryphosate kwa kunyunyizia.

"Mbali na viuatilifu hivyo tulivyogundua hivi karibuni pia wako wadudu maalum wanaozalishwa kwenye taasisi yetu wajulikanao kama 'Zygogramma Bicolorata' ambao tulitoa mbegu yake nchini Afrika kusini na tumeanza kusambaza maeneo mbali mbali nchini yenye kuathiriwa na mmea huu.

Awali akitoa taarifa za mmea huo, Mtafiti mwandamizi Ramadhani Kalewa alisema kuwa ulianza kuonekana nchini mwaka 2010 mkoani Arusha pembezoni mwa barabra ya Namanga-Arusha bila madhara yake kugundulika .

"Baada ya utafiti tukabainika kuwa na madhara makubwa hasa unapoingia mashambani kwa hudidimiza mazao na kupunguza kiwango cha ustawi na mavuno kwa asilimia 40 hadi 90 lakini pia huweza kuua mifugo wakiwemo mbuzi na kondoo ambao hawachagui majani ya malisho,"amesema.

Alisema kuwa kwa binadamu huleta mzio (allerg) endapo mmea huo ukigusana na ngozi huweza kusababisha magonjwa ya pumu ‘Asthma’ endapo akavuta vumbi la majani yake pamoja na kansa na ugonjwa wa macho ambao muathirika huwashwa na kuwa mekundu.

kwa upande wake Ofisa Mtafiti Mkuu kutoka TPHPA, Eliningaya Kweka amesema katika mafanikio hayo, pia wamenunua vifaa mbali mbali vya kubaini mimea vamizi na njia za kuzidhibiti kabla hazijaleta madhara nchini.

Aidha, Kweka alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakulima kutoa taarifa za haraka wanapobaini kuwepo na mimea vamizi ambazo bado hazijafahamika viuatilifu vya kuviangamiza na sisi tutawapa suluhisho kabka haijaleta madhara.