Watafiti waja na mbegu zinazokabili ukame
Muktasari:
Watafiti wa mbegu za mahindi nchini wamekuja na mbegu mpya ya mahindi aina ya Selian H115 ambayo inatarajiwa kumsaidia mkulima kukabiliana na ukame unaotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Arusha. Watafiti wa mbegu za mahindi nchini wamekuja na mbegu mpya ya mahindi aina ya Selian H115 ambayo inatarajiwa kumsaidia mkulima kukabiliana na ukame unaotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Akizungumzia mbegu hiyo, Mratibu msaidizi wa mahindi Kitaifa na Mkuu wa kitengo cha mbegu za mahindi kutoka Taasisi ya utafiti wa Kilimo (TARI-Selian), Zablon Msengi amesema mbegu hiyo inahitaji mvua chache na mavuno yake ni mengi.
Msengi amesema mbegu hiyo ina uwezo wa kutoa gunia 33 za mahindi kwenye ekari moja endapo mkulima atazingatia kilimo bora na utunzaji wote wa kitaalamu.
Pamoja na mbegu hiyo amesema zipo aina nyingine za mbegu za mahindi ambazo ni Vumilia K1 na Stuka M1 ambazo zina uwezo wa kuvumilia ukame na uhitaji wake wa mvua ni kuanzia milimita 300 hadi 400 badala ya milimita 800 hadi 1500 za mvua.
"Hapa Selian tunazo aina 11 za mbegu za mahindi ambazo tunazitafiti kulingana na matakwa ya nchi na wananchi kwamba wanataka nini maana mahindi ni zao linalolimwa karibia robo tatu ya nchi na sisi tumekuwa tukitafuta sifa ambazo wakulima wanazipenda ili tuweze kukidhi matakwa yao,
"Hali ya hewa ya nchi yetu na dunia kwa ujumla mvua sio nzuri na kwasababu nchi yetu inategemea mvua kwenye kilimo tukaona tufanyeje kama watafiti, tukaja na mbinu ya kutafuta mbegu ambazo zinavumilia ukame ili mkulima akilima kwa kutumia hiyo mvua kidogo aweze kupata mavuno angalau ya kutosha," amesema Msengi na kuongeza
“Hapa Selian tuna mbegu vumilia K1 na nyingine inaitwa Stuka M1 kwa ajili ya kumsaidia mkulima kulingana na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na Selian H115 ambayo ni suluhisho kubwa kwa wakulima wetu,"