Wataka bima ya afya ihusishe taulo za kike
Muktasari:
- Unyanyapaa kwa wasichana wakati wa hedhi, umetajwa kuwa moja ya mambo yanayoweza kuwaathiri kisaikolojia.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetakiwa kuandaa mpango utakaojumuisha upatikanaji wa taulo za kike katika bima ya afya, hasa kwa wanawake wanapokwenda kupata matibabu hospitali.
Kwa mujibu wa wadau, hatua hiyo itawaepusha wanawake na changamoto zinazotokana na upatikanaji wa taulo za kike zinazosababishwa na mambo mbalimbali.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Agosti 22, 2024 na Katibu wa Jukwaa la Hedhi Salama Tanzania, Severine Allute wakati wa hafla kutambulisha kitabu cha Shangwe kinachoelezea maisha ya binti katika rika balehe.
Katika hotuba yake kwenye uzinduzi huo, amesema Wizara ya Afya ndiyo inayopaswa kuandaa mpango huo ili kuwezesha upatikanaji wa taulo hizo kwa wasichana hasa wa rika balehe.
Sambamba na hilo, ametaka jamii ishirikiane katika juhudi za kumlinda mwanamke na hedhi salama, huku akisisitiza iepuke kuwanyanyapaa watoto wa kike wanapokuwa kwenye hedhi.
Kwa mujibu wa Severine, unyanyapaa wa wanawake hasa wa rika balehe wakati wa hedhi pamoja na athari nyingine, pia unawaathiri kisaikolojia.
Katika hafla hiyo iliyoambatana na uzinduzi wa taulo za kike za kampuni ya Pacify ametaka wanaume pia washiriki kuwezesha mabinti katika hedhi salama.
Daktari kutoka Hospitali ya Aga Khan, Jane Muzo amesema wakati wa hedhi binti huwa na mahitaji kadhaa na asipoyapata mara nyingi huathirika kisaikolojia.
“Tunavyosema hedhi salama ni mahitaji muhimu ambayo mtoto wa kike anatakiwa kuyapata wakati wake wa hedhi ni pamoja na taulo za kike, mazingira safi ya kubadilisha na kuweka taulo hizo na ushiriki wa karibu kutoka kwa wazazi hasa wakina mama,” amesema.
Joseph Muna Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hio, amesema wanatarajia kuandaa tukio la hisani kwa kushirikiana na waandishi wa kitabu cha Shangwe. Linatarajiwa kufanyika Agosti 30, 2024 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibasila jijini Dar es Salaam.
Amesema tukio hilo, litajumuisha majadiliano na wataalamu wa afya na ushuhuda kutoka kwa wanawake waliotumia taulo za kike za Pacify.