Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi waomba Serikali iweke mpango wa taulo za kike shuleni

Sehemu ya wanafunzi 400 wa shule ya Sekondari Mkonoo iliyoko kata ya Muriet waliopatiwa msaada wa Taulo za kike kupitia kampeni ya 'Her Needs Tanzania'. Picha na Bertha Ismail

Muktasari:

  • Wanafunzi wa shule za sekondari wanaoishi kwenye jamii za pembezoni wameiomba Serikali kuwawekea mpango wa taulo za kike shuleni ili ziwasaidie kujisitiri lakini pia kuhudhuria masomo yao kwa uhuru.

Arusha. Wanafunzi wa shule za sekondari kutoka jamii za pembezoni wameiomba Serikali kuwawekea mpango wa taulo za kike shuleni kuwasaidia kujisitiri ili waweze kuhudhuria masomo kwa uhuru.

Ombi hili limetolewa leo, Agosti 10, 2024, wakati wa kupokea msaada wa taulo za kike 400 kutoka kwa mtoto Arjun Kaur Mittal (16), kupitia kampeni yake ya 'Her Needs Tanzania', yenye lengo la kuwafikia wanafunzi zaidi ya 10,000 mkoani Arusha.

Makamu wa Rais wa Shule ya Sekondari Mkonoo, Anna Temba amepokea taulo hizo na kuishukuru Serikali, akisisitiza umuhimu wa kuingiza taulo hizo kwenye mpango wa vifaa vya shule vinavyopelekwa shuleni.

"Kama Serikali inavyoona umuhimu wa kutuletea vifaa vya kujifunzia kama vile maabara, vitabu na walimu, pia tunaomba iongeze taulo za kike. Hii ni kwa sababu zote zina lengo la kukuza kiwango cha taaluma cha mwanafunzi. Wasichana wengi wanapokuwa kwenye hedhi hushindwa kuhudhuria masomo kwa uhuru," amesema Temba.

Ameongeza kuwa familia nyingi hasa za pembezoni ziko katika hali duni kiuchumi na hazina uwezo wa kununua taulo hizo kila mwezi, hivyo wengi hulazimika kutumia vitambaa ambavyo vinawaweka katika hofu ya kuvuja, kuanguka hadharan, au hata kuwaletea maradhi kutokana na kuvivaa kwa zaidi ya saa 10.

Mtoto Mittal, akizungumza wakati wa kukabidhi taulo hizo, amesema ameamua kuchangisha fedha kwa marafiki na ndugu zake wanaoishi Dubai na India, pamoja na Arusha, baada ya kugundua changamoto kubwa wanayokumbana nayo wanawake wakati wa hedhi.

“Mimi nimezaliwa hapa Arusha na naona changamoto ninazopitia nikiwa kwenye siku hizo za hedhi, lakini nina uwezo wa kununuliwa taulo hizi.

“Nilipata picha ya wale walio katika familia duni hapa Arusha wasioweza kununua, nikajua uhitaji ni mkubwa na nikaamua kuomba msaada kwa marafiki, ndugu na jamaa. Nashukuru Mungu wameniunga mkono,” amesema Mittal.

Mittal amesema ameweza kuchangisha dola za Marekani 60,000 kutoka kwa marafiki aliosoma nao India na Dubai, ambazo anatarajia kusaidia zaidi ya wasichana 10,000 kwa awamu ya kwanza.

“Kupitia kampeni ya 'Her Needs Tanzania' ninayofanya kwenye mitandao ya kijamii, napata fedha za kununua taulo hizi. Kabla ya kuwapa, tunatoa elimu ya matumizi, hedhi salama na matumizi yake, lengo ni kuhakikisha mwanafunzi wa kike hakosi masomo kwa sababu ya changamoto hiyo,” amesema Mittal.

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, ameshuhudia hafla hiyo na kumpongeza Mittal kwa msaada huo.

Pia amewataka wadau wengine na mashirika kujitokeza kusaidia wasichana kujistiri kipindi chao cha hedhi.

“Elimu ni muhimu kwa watoto wetu, hasa wasichana ambao wanakuja kuhudumia jamii kubwa baadaye. Niombe wadau wengine wajitokeze kuunga mkono jitihada hizi ili kufanikisha wanafunzi wengi zaidi kufikiwa na msaada huu,” amesema Gambo.

Mwalimu wa Shule ya Mkonoo, Bernadetha Cosmas, amesema changamoto za hedhi zimeathiri baadhi ya wanafunzi kitaaluma kwa utoro au kuomba ruhusa na kukaa nyumbani kwa siku tano hadi 10 kila mwezi, jambo ambalo amesema linaweza kuondolewa na msaada huo.


Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.