Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti wabaini wasichana asilimia 75 wanapendelea taulo za kufua

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel akiwa na baadhi ya wanafunzi jijini Arusha.

Muktasari:

Wakati kukiwa na changamoto ya upatikanaji wa taulo za kike kwa kundi la wasichana waliopo mashuleni, utafiti mpya umebaini asilimia 75 ya waliopo vijijini wanapendelea taulo za kutumia na kufua 'reusable pads' hata hivyo hazipatikani sokoni.

Arusha. Asilimia 75 ya wanafunzi waliohojiwa katika baadhi ya shule za sekondari na msingi ndani ya mikoa 22 nchini, walionyesha kupendelea zaidi taulo za kike za kutumia na kufua, utafiti umebaini.

Majibu ya madodoso ya utafiti, wasichana hao wamesema taulo za kufua huokoa uchumi wa wazazi wao,  kutunza mazingira lakini pia huondokana na adha ya kukosa mahali pa kutupa pindi wanapomaliza kutumia.

Aidha wakati wa utafiti iligundulika kuwa wakati taulo za kuvaa na kutupa zikipatikana sokoni hadi vijijini, bado upatikanaji wa taulo za kuvaa na kufua  sokoni hasa vijijini ni changamoto.

Akitoa majibu ya utafiti huo leo Jumanne, Mei 28, 2024 kwenye maadhimisho ya siku ya hedhi salama, Mkurugenzi wa Oikos EA, Mary Birdi amesema utafiti huo umefanywa na Oikos, E-MAC Tanzania chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Amesema utafiti huo ulilenga kutathmini soko la taulo za kike katika shule za sekondari na msingi zilizopo maeneo ya vijijini.

Birdi amesema katika tafiti hiyo, waliangazia soko la vifaa vya afya ya hedhi na usafi ikiwamo ushuru, gharama, uwezo wa kumudu, ugavi na hatua stahiki mpaka kufika kwa walengwa.

"Utafiti umebaini wakati taulo za kuvaa na kutupa zikipatikana sokoni hadi vijijini, bado upatikanaji wa la taulo za kuvaa na kufua sokoni hasa vijijini ni changamoto. Hivyo basi mfumo ulioanzishwa kupitia mradi huu umehakikisha taulo za kuvaa na kufua zinapatikana hadi ngazi ya shule ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hizi kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla," amesema.

Amesema upembuzi huo pia ulibaini mlolongo mrefu na wenye gharama katika kurasimisha bidhaa za hedhi nchini, hivyo kusababisha uuzaji na uzalishaji holela wa bidhaa hizo usiozingatia taratibu za kiukaguzi katika kudhibiti ubora na usalama, lakini pia kuharibika kwa mnyororo wa usambazaji unaosababisha kuyumba kwa soko la bidhaa za hedhi.

Kilele cha maadhimisho ya juma la hedhi Salama Duniani, ambayo kitaifa yameadhimishwa jijini Arusha.

Baadhi ya wasichana wa shule za sekondari Mkoa wa Arusha waliosoma risala, walisema hedhi kwa wasichana wengi shuleni si salama.

Akisoma risala hilo, Anasia Cosmas amesema wasichana huingia gharama kununua taulo za kike kana kwamba wamekosea kuzaliwa wa kike.

"Gharama za taulo za kike zipo juu sana, hii inachangia afya za wasichana kuwa hatarini, hedhi salama inawezekana si tu kuondoa VAT bali kugawa taulo bure kwa wasichana waliopo shuleni inawezekana, tunamuomba Rais Samia aliangalie hili," amesema Anasia.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema suala hilo limechukuliwa na litaenda kufanyiwa kazi.

"Tulisema tuondoe VAT iliondolewa, lakini changamoto ikawa maeneo mingine kodi ilibaki palepale, tutaenda tena kuzungumza na Waziri wa Fedha kuhusu maombi haya na tutakuja na majibu sahihi," amesema Dk Mollel na kusisitiza;

"Kama tunanunua kondomu na kuziweka bure chooni na kwingine kwanini tusiweke pedi vyooni hasa kwa wanafunzi, punguzeni vikao hizi fedha ziende kununua pedi."

Akitoa hotuba yake katika maadhimisho hayo, Dk Mollel amewataka wazazi na walezi nchini, kuhakikisha  wanawawezesha watoto wa kike  kila mwezi kupata vifaa vyao vya kujilinda na kuwa na hedhi salama katika muda husika.

"Wazazi mara nyingi tumekuwa tukitenga bajeti ya kununua vitu mbalimbali kwa ajili ya matumizi majumbani kwetu lakini eneo hili la kununua pedi ‘taulo za kike’ mara nyingi tunalisahau.

"Niwaombe wazazi na walezi wote tutenge bajeti ya kila mwezi, kwa ajili ya kuwezesha hawa mabinti zetu wawe na uhakika wa kuwa na taulo za kike na kufikia malengo ya hedhi salama” amesema Dk Mollel.

Amesema Serikali imekuwa ikihimiza uwekezaji wa uzalishaji bidhaa za hedhi nchini, ili ziweze kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu. Hata hivyo amepongeza mchango wa wadau wa Sekta katika kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa taulo hizo.

Naye Mwakilishi wa Mkoa wa Arusha Dk Omary Chande, akitoa salaamu za mkoa, amesema mkoa  wa Arusha ni miongoni mikoa iliyopokea fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza afua za afya.

"Katika mwaka wa fedha 2023/24 mkoa ulipokea zaidi ya Sh33.2 bilioni za uboreshaji wa miundombinu ikiwemo Hospitali ya Mkoa, Wilaya na vituo vya afya," amesema Dk Chande.

Juma la Hedhi salama ambalo lilianza Mei 25, 2024 na kuongozwa na Kaulimbiu "Kwa pamoja Tuweke Mazingira Rafiki na Endelevu kwa Hedhi Salama" limefikia mwisho leo kwenye viwanja vya Makumbusho ya Mnara wa Mwenge jijini Arusha.