Wataka Serikali itoe takwimu za corona

Muktasari:

  • Wakati Watanzania wakiendelea kujitokeza kapatiwa chanjo ya Covid-19 katika mikoa yote nchini, baadhi yao wameitaka Serikali kutoa takwimu zinazoonyesha ukubwa wa tatizo ili waendelee kuchukua tahadhari.


Dar/Mikoani. Wakati Watanzania wakiendelea kujitokeza kapatiwa chanjo ya Covid-19 katika mikoa yote nchini, baadhi yao wameitaka Serikali kutoa takwimu zinazoonyesha ukubwa wa tatizo ili waendelee kuchukua tahadhari.

Takwimu za mwisho zilitolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima Julai 23, 2021, kulikuwa na jumla ya vifo 29 vilivyosababishwa na wimbi la tatu huku kukiwa na wagonjwa 858 wa Covid-19.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti walisema, kitendo cha viongozi wa Serikali kutotoa takwimu kinaipa jamii viashiria kwamba tatizo si kubwa hivyo wengi wao hawaoni umuhimu wa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka au vitakasa mikono sambamba na kutoepuka mikusanyiko.

Mkazi wa Mbagala Kizuiani, Geofrey Swai, alisema kutokana na kutokuwepo taarifa zinazotangazwa hasa idadi ya wagonjwa na wale wanaofariki kwa corona, inakuwa vigumu kwao kuchukua tahadhari na wanahisi tatizo hilo linakuzwa tu.

Mwananchi ilifanya uchunguzi na kubaini kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wenye matatizo ya upumuaji ambao wamekuwa wakihudhuria kwa wingi katika hospitali za umma na binafsi.

Hata hivyo baadhi ya hospitali zilikiri kuwa na ongezeko hilo na kwamba wamekuwa wakilazimika kutumia vyumba vya wagonjwa mahututi kulaza kundi hilo, hali ambayo isipodhibitiwa kwa hatua zaidi kuchukuliwa huenda ipo siku wagonjwa watakosa huduma ya oksijeni. Licha ya hali hiyo, daladala zimeonekana kujaza sana pasipo hatua za kujikinga kama ilivyoelekezwa hasa za Mbagala na Temeke na zile za Mbezi, huku hali ikiwa tofauti na daladala zinazofanya safari zake Makumbusho kwenda Posta na Gerezani.


Katika stendi za daladala na magari yaendayo pembezoni Mbagala, hakukuwa na mapipa ya maji ya kunawa na sabuni katika maeneo ya kuingia na kutokea.

Meneja wa stendi hiyo, Mgalula Mlingilili alisema “Matenki kwa ajili ya kunawa bado hatujaweka lakini yalikwenda kutengenezwa tunaamini yatarejeshwa leo na kesho watu wataanza kunawa.”

Katibu wa umoja wa madereva na makondakta wa mabasi, Lazaro Mwaja alisema utekelezaji unakuwa mgumu kutokana na bei ya mafuta kuwa juu.

Maelfu wajitokeza kuchanjwa

Wakazi wa Dodoma wameendelea kujitokeza katika vituo 28 vya mkoani humo ilianza juzi ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka alizindua kwa kuchanja katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo.

Mwananchi lilitembelea jana katika vituo vya kutolea chanjo hiyo cha Kituo cha Afya cha Makole, Hospitali Teule ya Wilaya ya St Gema na kukuta foleni ya watu wakisubiri kupata huduma hiyo.

“Nimekuja hapa saa 11.00 asubuhi nikafanya taratibu za kuandikisha ndio natoka hivi sasa kuchanja. Kwa kweli wenye kuelewa wataendelea kuchanja,” alisema Nelly Nyamhula.

Katika Wilaya ya Mpwapwa, Mratibu wa chanjo wilaya hiyo Fulgence Temu aliwataka watu kuondoa shaka chanjo hiyo ni salama na haina madhara kwa afya ya binadamu .

Alisema kwa Mpwapwa wamepokea chanjo zaidi ya 4,000 ambazo zitatawanywa katika vituo vitatu vya kutolea chanjo ambavyo ni Hospitali ya wilaya Mpwapwa, kituo cha Afya Kibakwe na kituo cha afya Mtera.

Imeandaliwa na Herieth Makwetta, Sharon Sauwa, Lwitiko Mwamakua, Alodia Dominick na Samirah Yusuph.