Wataka wachimba madini waondolewe Mto Ruvu

Muktasari:

  • Serikali ya kijiji imeomba kuongezewa nguvu kuwaondoa wachimba madini kando mwa Mto Ruvu.

Morogoro. Viongozi wa Kijiji cha Kibangili wilayani Morogoro wameiomba Serikali kuongeza nguvu ya kukomesha uchimbaji madini kwenye kingo za Mto Ruvu unaokatiza katika ya kijiji hicho kwa kuwa Serikali ya kijiji imeshindwa.

Ombi hilo limetolewa na ofisa mtendaji wa Kijiji cha Kibangili, Hamis Kibwana alipotoa taarifa ya uharibifu wa kingo za mto huo unaofanywa na wachimbaji madini.

Amesema hayo mbele ya wadau wa maji kutoka Bonde la Wami Ruvu na Wizara ya Maji na Umwagiliaji wakati wa ziara kukagua mradi wa uhifadhi wa vyanzo vya maji kupitia usimamizi wa matumizi bora ya ardhi kwenye Bonde la Mto Ruvu na Zigi.

Ofisa mtendaji huyo amesema wachimbaji hao walishapewa notisi ya kuondoka, hata hivyo wanaendelea na shughuli za uchimbaji.

Amesema walishafanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulinda maeneo yote ya mto huo yanayochimbwa madini na kutoa elimu ya namna ya kuhifadhi kingo lakini kasi ya uchimbaji imekuwa ikiongezeka na kuhatarisha usalama.

Ofisa maji kutoka Bonde la Wami Ruvu, Plaxeda Karugendo amesema katika kulinda na kutunza kingo na vyanzo vya maji, ofisi ya bonde hilo imekuwa ikishirikiana na jumuiya za watumia maji katika vijiji na kutoa elimu ya ufugaji nyuki itakayosaidia kuhifadhi mazingira yaliyo jirani na mito.

Hata hivyo, amesema changamoto kubwa ni uelewa kwa baadhi ya jamii kwa kuwa mbali ya uchimbaji madini, pia kumekuwa na shughuli za kilimo kando ya mito na uingizaji wa mifugo  mtoni.