Watakiwa kutumia fursa soko la parachihi
Muktasari:
- Wakati kukiwa na mahitaji makubwa ya parachichi nje ya nchi, uzalishaji wa zao hilo nchini bado uko chini.
Arusha. Wakulima wa zao la parachichi Kanda ya Kaskazini wametakiwa kutumia fursa ya kuzalisha zao hilo kwa wingi kutokana na uhitaji mkubwa wa mafuta yatokanayo na zao hilo katika nchi za Mashariki ya kati.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi 29 jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayozalisha mafuta ya Parachichi, Avomero group Limited, Jesse Oljange, amesema kwa sasa wanasafirisha mafuta ghafi nje ya nchi kwa asilimia 90 ambapo mafuta hayo yamekuwa yakitengeneza vipodozi.
"Soko linahitaji mafuta mengi kuliko uwezo wetu wa uzalishaji, maana kwa mwaka tunazalisha kwa siku 120 tuu, hivyo tunaangalia ni namna gani ya kukidhi soko hili,” amesema.
Amesema kwa upande wa Kanda ya Kaskazini mpaka sasa wapo wakulima wa parachichi 8,400 ambapo tayari vikundi 271 kati vikundi 487 vimeshaunganishwa na teknolojia kwa ajili ya kuzalisha na kuchakata zao hilo hasa kwenye maeneo ya vijijini.
"Tangu mwaka 2017 tulivyoanza kuunda vikundi vinavyozalisha zao la parachichi tuna vikundi 487 maeneo ya vijijini, ambapo tayari 271 vimefikiwa na teknolojia ya uchakataji wa zao hilo na kwa sasa wakulima 8,400 tayari wameshapata faida kutokana na zao hili.
"Mashine ambazo tumezifunga kwenye maeneo ya vijijini zimeonekana kwa siku mashine ndogo inazalisha tani nne ya mafuta na mashine kubwa inazalisha tani saba za mafuta kwa siku, hii ni fursa kwa wakulima kujikita zaidi kwenye uzalishaji wa zao hili kwani lina manufaa makubwa," amesema.
Nao baadhi ya wakulima wa zao hilo, wamesema wameweza kujikwamua kiuchumi na kuweza kuziendesha familia zao kutokana na zao hilo ambalo limekuwa ni mkombozi wa maisha yao ya kila siku.
Amani Tesha, ambaye ni mkulima na mnufaika wa zao hilo amesema kilimo cha parachichi kimekuwa na manufaa makubwa kutokana na zao hilo kuongezewa thamani ambapo wameweza kufungiwa mashine kwa ajili ya kuchakata zao hilo.
"Tunaishukuru Avomero kwa kutufungia mashine katika maeneo yetu kwa ajili ya kusindika na kuchakata zao hili la parachichi, tumeona manufaa makubwa katika zao hili maana tumeweza kuboreshewa miundo mbinu na tumeweza kufanya vizuri," amesema.