Watano wasimamishwa kazi tuhuma kifo cha mjamzito aliyewekewa damu isiyo sahihi

Muktasari:

  • Watumishi watano wa Kituo cha Afya cha Mikanjuni Mkoa wa Tanga wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa kifo tata cha mjamzito kinachodaiwa kusababishwa kwa kuongezewa damu asiyostahili.

Tanga. Mkuu wa Wilaya ya Tanga, James Kaji ameagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi watano wa Kituo cha Afya cha Mikanjuni kwa kutuhumiwa kuhusika na kifo cha mjamzito Fatma Mussa (36) kilichotokea Jumatano ya Machi 27, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumamosi Machi 30, 2024, DC Kaji amesema katika wodi aliyokuwa amelazwa marehemu, kulikuwa na mgonjwa ambaye alihitaji kuwekewa damu na damu yake ilikuwa tayari imeandaliwa.

Hivyo muuguzi aliyekuwa zamu alimwekea marehemu ambaye alikuwa ni mjamzito damu ambayo hakustahili kupewa na hakuwa na uhitaji huo, hali  iliyomsababishia mzio mkali na hivyo kuchangia kifo chake.

Amesema awali alipofikishwa katika kituo hicho cha afya, marehemu alifanyiwa upasuaji na kufanikiwa kupata mtoto wa kike aliyekuwa na uzito wa kilo tatu na wala hawakuwa na tatizo lolote lile.

Mkuu huyo wa wilaya amewataja watumishi wanaotakiwa kusimamishwa kazi na Ofisi ya Mkurugenzi wa  Jiji la Tanga ili kupisha uchunguzi,  ni muuguzi Fadhila Ally, Restitua Kasendo na Muya Ally Mohamed pamoja na madaktari Andrew Kidee na Hamis Msami.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Fredrick Sagamiko amesema tayari watumishi hao wamesimamishwa kazi na uchunguzi utafanyika na endapo wakigundua tatizo lolote la ukiukwaji wa taratibu za kazi watumishi hao watachukuliwa hatua.

Akielezea mkasa huo, mume wa marehemu, Rashid Juma ameiomba Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya waganga na wauguzi waliosimamia upasuaji wa mke wake na kuzembea hadi kufariki kwake.

Amesema mkewe alifikishwa Kituo cha Afya Mikanjuni Machi 27, 2024 kwa ajili ya kupata huduma ya kujifungua ila baadaye alipata taarifa amefariki dunia huku kifo chake kikiwa na utata.

Juma amesema alifichwa taarifa ya kifo cha mkewe kutokana na mazingira ambayo wao waliona hawawezi kumwambia, hivyo yeye alitaarifiwa na ndugu zake baadaye kuwa mkewe amefariki dunia.

"Sikuwa na taarifa kuhusu kifo cha mke wangu, nilikwenda nyumbani kwa baba mdogo ili kutoa taarifa ya ugonjwa ila kufika kule kumbe walinificha baadaye ndio nikaambiwa mgonjwa amefariki dunia kwakweli niliishiwa nguvu," amesema Rashid.

Dada wa marehemu, Dhamana Bakari amesema wakati akiwa kituo hicho cha afya aliambiwa akae nje na mtoto ila kutokana na mazingira ya hapo aliomba amchukue mtoto na kurudi naye nyumbani.

Amesema wakati anafika nyumbani na mtoto ndio akapewa taatifa ya kifo cha mgonjwa kwa madai wauguzi walishindwa kumpa hiyo taarifa kuwa mgonjwa wake amefariki dunia.