Watumishi wa afya wapigwa marufuku ‘kuchati’ kazini

Muktasari:

  • Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amesema kuna malalamiko mengi kuwa watumishi wa afya ‘wanachati’ na kufanya mawasiliano binafsi badala ya kuwahudumia wagonjwa.

Dodoma. Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amepiga marufuku watumishi wa sekta ya afya nchini ‘kuchati’ kwa kutumia simu zao wakiwa kazini, kwa kuwa wako mahali hapo kutoa huduma kwa wananchi.

Ametoa agizo hilo leo kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu huduma duni katika vituo vya afya, ambako watumishi hao wamekuwa wakitumia muda mrefu kufanya mawasiliano binafsi badala ya kuwahudumia wagonjwa.

Profesa Nagu ametoa agizo hilo leo Januari 26, 2024 alipozungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure mkoani Mwanza, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, iliyolenga kukagua mikakati ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu.

“Ni marufuku kutumia simu zetu kuchati kwa sababu tunapokuwa kwenye zamu, chochote kinaweza kikatokea.

“Mgonjwa anakuwa hajaruhusiwa kukaa nyumbani kwa nini, ni kwa sababu yupo (hospitali) kwa ajili ya uangalizi. Ingekuwa haihitaji uangalizi tungemwambia nenda nyumbani,” amesema.

Profesa Nagu alisisitiza umuhimu wa watumishi wa afya kuzingatia majukumu ya kitaalamu wakiwa kazini ili kuhakikisha wanatoa huduma bora na zenye ufanisi kwa wananchi.

Mganga mkuu huyo aliwataka watumishi wa sekta hiyo kubadilika, kuwapenda watu na kuipenda kazi yao na kwa kufanya hivyo wataifurahia kazi yao.

“Angalieni viapo vyetu vinasema nikifanya haya (nitabarikiwa), lakini ninajua kuwa kinyume chake usipofanya haya ni laana, sasa mchague, wenyewe mnataka kubarikiwa au mnataka laana,” amesema.

Pia amesema atahakikisha huduma za afya zinaboreshwa na wananchi wanapata huduma bora na za haraka wanapozihitaji, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.


Aliyedaiwa kutelekeza mjamzito huru

Wakati huohuo, Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) limemwachia huru muuguzi na mtaalamu wa idara ya usingizi na ganzi katika Kituo cha Afya cha Kabuku, Wilaya ya Handeni, Mussa Yusuph baada ya kushindwa kumtia hatiani kwa tuhuma za kumtelekeza mjamzito.


Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), Profesa Lilian Msele (kulia) akisoma hukumu ya wauguzi waliotuhumiwa kwa makosa mbalimbali, (kushoto) ni Msajili wa baraza hilo, Agness Mtawa.


Mbali na hilo, TNMC imewasimamisha kutoa huduma ya uuguzi na ukunga kwa mwaka mmoja, wauguzi wawili wa Halmashauri ya Bunda mkoani Mara kwa makosa mawili, likiwemo la kuharibu na kupoteza nyaraka zilizotumika kumhudumia mgonjwa.

Kuhusu tukio la Muheza, Novemba 27, mwaka jana, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitoa siku 14 kwa baraza hilo kutoa taarifa ya hatua ilizomchukulia Yusuph baada ya kamati ya kuchunguza kifo cha mjamzito Mariam Zahoro kumkuta na makosa ya kiutendaji wakati akitoa huduma.

Mjamzito huyo alifariki dunia Novemba 11 mwaka jana wakati akipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Kabuku kwa kilichoelezwa kuwa ni kukosa Sh150,000 kwa ajili ya upasuaji.

Akizungumza jana jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Baraza hilo Profesa Lilian Msele alisema jumla ya wauguzi saba walifikishwa katika baraza hilo kwa tuhuma mbalimbali akiwemo Yusuph aliyetuhumiwa kwa kumtelekeza mgonjwa na kushindwa kumpatia dawa ya usingizi.

“Baada ya kusikilizwa (yeye) na mashahidi na vielelezo, baraza halikumtia hatiani na hivyo lilimwachia huru kuendelea na kazi zake za utumishi wa umma,” amesema Profeza Msele.


Wauguzi wanne watiwa hatiani

Profesa Msele alisema wauguzi wanne wa Halmashauri ya Bunda mkoani Mara wametiwa hatiani kwa makosa tofauti likiwemo la kuharibu na kupoteza nyaraka zilizotumika kumhudumia Neema Joseph, mjamzito aliyefariki dunia kwa kupoteza damu nyingi.

Amesema Nyasigwa Seba, amepewa onyo kali baada kushindwa kutoa taarifa katika Kamati ya Uongozi ya Mkoa kama taratibu zinavyotaka kuhusu kifo cha mjamzito huyo.

Mwingine ni Mratibu wa Mama na Mtoto katika Halmashauri ya Bunda, Mrimi Baritwa aliyedaiwa kuharibu na kupoteza nyaraka zilizotumika kumhudumia mgonjwa na kushindwa kutoa taarifa kwenye uongozi wa mkoa kwa mujibu wa taratibu .

“Baraza lilimsikiliza na kumtia hatiani na hatimaye kupewa adhabu ya kusimamishwa huduma za uuguzi na ukunga kwa muda wa mwaka mmoja,” alisema.

Beatrice Joseph, amepewa onyo na baraza hilo baada ya kutiwa hatiani kwa kushindwa kutoa taarifa kwa uongozi wa mkoa kuhusu kifo cha Neema.

Muuguzi Kiongozi wa Halmashauri ya Bunda, Suzan Sarongo naye alituhumiwa kwa kuharibu na kupoteza nyaraka zilizotumika kumhudumia mgonjwa na kushindwa kutoa taarifa kwenye kamati ya uongozi ya uchunguzi ya mkoa kuhusu kifo cha mjamzito huyo.

“Baraza lilimtia hatiani na kupatiwa adhabu inayohusisha kutokutoa huduma ya uuguzi na ukunga kwa muda wa mwaka mmoja,” amesema.


Wawili wapewa onyo

Profesa Lilian alisema wauguzi wawili wa ngazi ya cheti wa Halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga, walipewa onyo kali na baraza baada ya kutiwa hatiani.

Amewataja wauguzi hao kuwa ni Zabibu Mwaji na Agnes Michael, ambao walituhumiwa kushindwa kudumisha viwango vya utoaji huduma, hivyo kusababisha madhara kwa mgonjwa.

Agnes pia alituhumiwa kwa kosa lingine la kushindwa kutoa usaidizi wa kitaaluma kwa msaidizi aliye chini yake kinyume cha utaratibu, akiwa kiongozi wa eneo la utoaji wa huduma.


Katika tukio jingine, Ofisa Muuguzi Msaidizi, Elias Msese kutoka Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora amesimamishwa kutoa huduma ya uuguzi na ukunga kwa miezi sita baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kufanya upasuaji wa mshipa wa ngiri nje ya mipaka ya leseni yake.


Profesa Lilian alisema pia muuguzi huyo alitiwa hatiani kwa kushindwa kudumisha viwango vya huduma na kanuni za maadili ya taaluma.


Mwingine nje miezi sita

Hata hivyo, alisema hawakuweza kumtia hatiani kwa tuhuma za kupokea fedha kutoka kwa ndugu wa mgonjwa kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa kudhibitisha kosa hilo.