Watatu wafariki Manyara, ajali ikihusisha magari matano
Muktasari:
- Ajali imetokea eneo la Mogitu wilayani Hanang' ambako awali kulitokea ajali nyingine.
Hanang'. Watu watatu wamefariki dunia na wengine watano wamejeruhiwa kwenye ajali iliyohusisha magari matano na pikipiki, eneo la Mogitu wilayani Hanang' Mkoa wa Manyara.
Ajali hiyo imetokea eneo la mteremko wa Mogitu katika barabara kuu ya Singida-Babati. Eneo hilo kulikuwa kumetokea ajali nyingine iliyohusisha magari mawili ya mizigo iliyosababisha njia kufungwa na magari kushindwa kupita, hivyo kusababisha basi la abiria kampuni ya Arusha Express yenye namba T162 AGB kukosa mwelekeo na kugongana na kugonga gari dogo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), George Katabazi akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Juni 10, 2024 amesema ajali hiyo imetokea saa saba usiku, Juni 9, 2024 wakati gari hilo la mizigo lilipokuwa likipanda Mlima Mogitu.
Katabazi amesema waliofariki ni watu watatu akiwemo mwanamke mmoja na majeruhi watano ambao bado wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang' (Tumaini).
"Dereva wa basi hilo la Arusha Express lililokuwa linatokea mjini Bukoba kwenda jijini Arusha, naye ni miongoni mwa abiria waliojeruhiwa na kukimbizwa hospitali," amesema Kamanda Katabazi.
Amesema kabla ya basi hilo la Arusha Express kupata ajali kulikuwa na ajali nyingine eneo hilo, hivyo kusababisha upande mmoja kutotumika ili kusaidia majeruhi.
"Ajali ya awali ilipotokea baada ya lori aina ya Scania kuligonga gari lingine na pikipiki, hivyo kusababisha kuziba upande mmoja wa barabara," amesema kamanda Katabazi.
Mmoja wa abiria aliyekuwa kwenye basi hilo, Amos Rushaiya, amesema dereva wao hakutambua kama eneo hilo kuna ajali, hivyo naye akajikuta ameingia kwenye mkumbo huo.
Amesema wanamshukuru Mungu wamenusurika kwenye ajali hiyo iliyosababisha vifo hivyo na majeruhi.