Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watatu washikiliwa mauaji ya mzee wa miaka 72 Kilimanjaro

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa

Muktasari:

  • Jeshi la polisi Mkoani Kilimanjaro, linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Isaack Mallya (72), mkazi wa Kijiji cha Umbwe Onana, Kata ya Kibosho Magharibi, Wilaya ya Moshi mkoani hapa.

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro, linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Isaack Mallya (72), mkazi wa Kijiji cha Umbwe Onana, Kata ya Kibosho Magharibi, Wilaya ya Moshi.

 Mwili wa Mzee Mallya, ulikutwa jana Desemba 2, 2024 umetelekezwa nje ya nyumba yake ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kukamatwa watuhumiwa hao leo Desemba 3, mwaka huu.  Kamanda Maigwa amesema chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika na kwamba wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.

"Tunawashikilia watuhuhumiwa watatu kuhusiana na mauaji ya mzee wetu, tunaendelea kuwahoji ili kubaini chanzo cha mauaji hayo," amesema Kamanda Maigwa.

Kaka wa marehemu, Patrick Boisafi ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, jana alieleza kusikitishwa na ukatiki aliofanyiwa kaka yake huyo na kusema wameliachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wake ili kubaini waliohusika na sheria ichukue mkondo wake.

Mbali na tukio hilo la kuuawa kwa kaka yake, Boisafi amekumbushia tukio la nyuma la kuuliwa kwa ng'ombe wa marehemu na kueleza kuwa, huenda wakati huo walipanga kutekeleza mauaji hayo na kukosea katika kujipanga.

"Huyu ni kaka yangu, ni mtoto wa baba yangu mkubwa, tumeishi wote mji mmoja na mahali alipouawa ndipo nimekulia hapo, ni jambo la kikatili sana limefanyika katika jamii, lakini naamini jeshi la polisi litafanya bidii kuchunguza matatizo yaliyotokea na kuwatafuta waliohusika na jambo hili ili hatua za kisheria zichukue mkono wake"alisema Boisafi.

Ameongeza kuwa "Hata kama mtu ni mkorofi au nini, kitu kilichofanyika kinakemewa na kila mtu, yaani jambo lililofanyika ni jambo la aibu mtu kuamua kuchukua uamuzi wake kwenda kumuua mtu tena nyumbani kwake, hii inaumiza sana."

 Aidha amesema kitendo kilichofanyika hakikubaliki katika jamii na kinatia hofu kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka na kwamba hata kama walikuwa wanamdai wangesema walipwe kwa kuwa hakuna kitu chenye thamani kulinganisha na uhai wa mtu.

"Kama walikuwa wanamdai wangesema tungelipa, lakini kitu walichokifanya, kusema ukweli ni ukatili, tunakemea jambo hili na lisijirudie kwa watu wengine, ni jambo linalosikitisha sana kwani linajenga hofu hasa kipindi hiki ambacho tunaelekea sikukuu za mwisho wa mwaka," ameeleza Boisafi.

Amesema "Matukio haya yanayotokea yanatisha hata wale ndugu zetu na marafiki zetu ambao watasafiri kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi kuja Kilimanjaro na mambo kama haya yanatia doa Mkoa wa Kilimanjaro na jamii yote inayotuzunguka."