Watatu wauwawa kwa visu, mwingine ajinyonga kwa wivu wa mapenzi
Muktasari:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime na Rorya, Andrew Satta amesema chanzo cha moja kati ya matukio hayo ni ugomvi wa mapenzi na mengine mawili bado hayajajulikana vyanzo vyake.
Tarime. Watu watatu wamefariki dunia kwa kuchomwa visu katika katika matukio na nyakati tofauti wilayani Tarime, Mkoa wa Mara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime na Rorya, Andrew Satta amesema chanzo cha moja kati ya matukio hayo ni ugomvi wa mapenzi na mengine mawili bado hayajajulikana vyanzo vyake.
Amesema katika tukio la Juni 5, saa mbili usiku katika barabara ya Mogabiri, Kata ya Kenyamanyori wilayani Tarime, Daniel Masubo (20) mkazi wa Mogabiri alijeruhiwa kwa kuchomwa kisu shingoni karibu na koromeo na Steven Mniko (30) mkazi wa kijiji hicho ambaye naye alijeruhiwa kwa kisu shingoni.
Alisema kuwa Masubo alipoteza maisha katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime wakati akiendelea na matibabu na kwamba, chanzo cha tukio hilo ni kuwa alimgusa mtuhumiwa ndipo ukaibuka ugonvi wa kuchomana visu.
Mtuhumiwa amelazwa katika hospitali hiyo na atafikishwa mahakamani atakapopata nafuu.
Katika tukio jingine lililotokea Juni 3 kwenye Kitongoji cha Kitare, Kijiji cha Kimusi, Kata ya Nyamwaga wilayani humo, Gikaro Magaigwa (32) aliuawa kwa kuchomwa kisu tumboni na kiganja cha mkono wa kushoto na chanzo cha tukio hilo hakijajulikana na mtuhumiwa alikimbia na anatafutwa na polisi.
Tukio jingine ni la Kitongoji cha Bubiritocho katika Kijiji cha Borega “B”, Kata ya Mbogi ambako Gimonge Chacha (20) alijeruhiwa kwa kuchomwa kisu tumboni na baadaye kupoteza maisha akiwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Omari Juma amesema kabla ya mauti kumfika, Chacha alichomwa kisu akiwa harusini baada ya kumtania mtuhumiwa kuwa bibi harusi alikuwa mpenzi wake na alishampatia Sh5,000, hivyo atakuwa mpweke baada ya kuolewa.
“Walizidi kutaniana mwishowe ukaibuka ugomvi,” amesema mwenyekiti huyo.
Sata amesema tukio jingine ni mkazi wa Kitongoji cha Matoke katika Kijiji cha Mangucha, Kata ya Nyanungu wilayani humo, Lameck Makanga (45) kujinyongwa kwa kamba.
“Tunamshikilia mkewe Rhob Makanga (30) kwa mahojiano zaidi kwa kuwa taarifa za awali zinaonyesha walikuwa na ugonvi,” amesema.